Na Theonestina Juma,Bukoba
BAADHI ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari wilayani Chato mwaka huu wamelazimika kurudia darasa la saba kwa madai ya kutaka
kujiunga na shule maalumu zilizoko mbali na makwao.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Bi. Khadija Nyebo kwenye Kamati ya Ushauri wa Mkoa Kagera (RCC) ambayo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Business Times Ltd inayochapicha magazeti ya Majira, Business Times, Spoti Starehe, Bw. Rashid Mbuguni.
Bw. Mbuguni alikaribishwa na Mkuu wa Mkoa Kagera, Bw. Mohamed Babu kuwasilisha mpango mpya ya kampuni hiyo kupitia gazeti lake la Majira katika kuchangia na kuongeza ufanisi wa wadau katika maendeleo ya Mkoa wa Kagera.
Bi. Nyembo alilazimika kusema hivyo, baada ya Bw. Babu kuhoji sababu za wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni wakati wamefaulu.
Mkuu huyo wa wilaya ya Chato Bi. Nyembo alisema kati ya watoto 3,939 waliofaulu 600 hawajaripoti shuleni hadi sasa.
Alisema kutokana na hiyo uongozi ulilazimika kuanza kufanya uchunguzi ili kubaini ni wapi waliko, ambapo ilibainika kuwa baadhi yao wamerudia darasa la saba.
Jambo hilo lilimlazimu Mkuu wa mkoa, Bw.Babu kumwomba Ofisa elimu wa Mkoa, Bw. Florian Kimolo kulitolea maelezo kisheria.
Bw. Kimolo alisema hakuna sheria inayoruhusu mwanafunzi yeyote yule aliyefaulu ama kufeli elimu ya msingi kurudia tena darasa la saba.
Ofisa Elimu huyo alisema kwa walimu wanaofanya hivyo wanavunja sheria na watakaobainika kutoa nafasi kwa watoto hao watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande waje, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara, Bw. John Shimimana alisema serikali inatakiwa kuangalia ni namna gani inavyoweza kuanzisha vyuo vya ufundi kila wilaya ili kuwezesha kila mwanafunzi anayemaliza elimu ya sekondari kuwa na ufundi wake badala ya kukaa vijiweni kama inavyojitokeza kwa hivi sasa.
Akichangia hoja hiyo, Bw. Mbuguni alisema tatizo la watoto kama hao wa Chato kuamua kurudia darasa la saba linatokana na kuona shule wanazotakiwa kwenda ni mbaya, jambo ambalo ni changamoto kwa viongozi husika.
“Katika kikao hiki nimesikia mkijadili juu ya watoto waliofauliu kwenda sekondari wameamua kurudia darasa la saba, hili kweli ni changamoto … hili la watoto kukacha shule wanazotakiwa kwenda na kuamua kurudia elimu ya msingi, ni mtihani na ni changamoto kweli kweli.
"Kuna baadhi ya viongozi wanapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi…. Watoto hawa wanaona hizi shule wakopangiwa kwenda ni mbaya, lakini katika hili ni kunahitaji tu kujipanga kwani ni mtihani,” alisema.
Akizungumzia suala la maendeleo alisema watu binafsi au jamii hudhani maendeleo sio jukumu lao bali la serikali na viongozi wao, na hivyo huishia kubweteka na kuilalamikia serikali kwa matatizo yao huku wengine wakidhani kuwa mtaji ndio masingi wa maendeleo.
Alisema kwa sasa kinachohitajika ni kuamsha hamasa ya maendeleo na kurejesha matumaini katika jamii iliyokata tamaa kwa kumpa kila mtu fursa ya kuishi na kuchangia maendeleo ya jamii, ili kila mtu atambulike, aheshimike na kuthaminiwa.
Alisema kushirikisha jamii katika jitihada za maendeleo yao kwa kuibua matatizo na kero zao, ili ziweze kujumuishwa katika mipango ya wadau na kuainisha mipango ya wadau kwa lengo la kuleta matumaini katika jamii ili iweze kuthamini na kuheshimu jitihada za wadau wao na kujenga utamaduni endelevu.
No comments:
Post a Comment