Na Amina Athumani
CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimesema timu zinazotakiwa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Tanzania zitakazoshindwa kuthibitisha hadi Juni 20, mwaka
huu zitashushwa daraja na kuondolewa kwenye michuano hiyo.
Mashindano hayo yanatarajia kufanyika Julai 3, mwaka huu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha ambapo timu 18 zitachuana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CHANETA Rose Mkisi alisema taarifa za mashindano hayo zilitolewa tangu Februari, mwaka huu hivyo muda wa kuthibitisha hautaongezwa.
"Timu zote zinazotakiwa kushiriki mashindano haya ya Klabu Bingwa zinatakiwa ziwe zimethibitisha ifikapo Juni 20 ambayo siku ya mwisho wa kuthibitisha zaidi ya hapo timu tutaishusha daraja na tutaiondoa katika mashindano hayo," alisema Rose.
Alisema timu zilizomaliza kulipa ada ya pamoja na kurudisha fomu hadi sasa ni saba ambazo ni Filbert Bayi, Polisi Arusha, Polisi Mbeya, Hamambe Mbeya, Magereza Morogoro, JKT Ruvu na Tumbaku Morogoro.
Katibu huyo alisema timu zote zinatakiwa kufika Arusha Julai Mosi mwaka huu kwa ajili ya mkutano wa viongozi utakaofanyika Julai 2 kabla ya mashindano hayo kufanyika Julai 3, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment