16 June 2011

Simba matumaini kibao Congo

*Yatamba kuvunja rekodi

Na Zahoro Mlanzi

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa, timu ya Simba inatarajia kuondoka leo nchini kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC), kuumana na DC Motema Pembe na kutamba inakwenda kuvunja rekodi ya timu hiyo ya kutofungwa nyumbani.

Mchezo huo ni wa marudiano wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho (CAF), ambapo mchezo wa awali uliopigwa wiki iliyopita Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' alisema maandalizi yanaendelea vizuri na hawana majeruhi mpaka sasa.

"Timu iliendelea na kambi kama kawaida mara baada ya mchezo ule dhidi ya Motema Pembe, ambapo ilikuwa ikifanya mazoezi Uwanja wa TCC, Sigara jijini Dar es Salaam na tunatarajia kuondoka kesho (leo) kabla ya saa sita mchana," alisema Kaburu.

Alisema kutokana na maandalizi waliyofanya ana imani wataibuka na ushindi katika mchezo huo na pia Kocha Mkuu, Mosses Basena ameshafanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mchezo uliopita.

"Tumesikia wapinzani wetu (Motema Pembe), tangu waanze mashindano haya hawajafanya vibaya katika uwanja wao wa nyumbani, hivyo sisi tunataka kwenda kuweka historia katika uwanja huo kwa kuifunga na kuingia hatua ya makundi," alitamba Kaburu.

Alisema taratibu zingine za safari wanaendelea kuzikamilisha ambapo wakiwa nchini humo watatumia siku mbili zaidi kujiandaa.

Kaburu alisema anawaomba Watanzania waliopo katika jiji la Kinshasa nchini na wa hapa nchini kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao, ambapo kwa mashabiki wa Tanzania wanaweza kulipia za ya dola 963 kusafiri Congo.

Wachezaji wanaotarajia kuondoka leo ni makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha 'Barthez', mabeki ni Salum Kanoni, Amir Maftah, Juma Jabu, Kelvin Yondani na Juma Nyosso, viungo ni Amri Kiemba, Jerry Santo na Shija Mkina.

Wengine ni nahodha Nicco Nyagawa, Mohamed Banka na Aziz Gila na washambuliaji ni Ally Ahmed 'Shiboli', Mussa Hassan 'Mgosi' na Emmanuel Okwi.

Simba ikifanikiwa kufuzu hatua hiyo itaingia moja kwa moja Kundi B, lenye timu za Sunshine ya Nigeria, Maghreb de Fes ya Tunisia na JS Kabylie ya Morocco.

No comments:

Post a Comment