*Wapanga kima cha chini shilingi 315,000
*Wazee wote nchini sasa kulipwa pensheni
*Waweka fumula kupunguza kodi ya mshahara
Na Tumaini Makene
IKIWA ni siku ya kwanza kwa wabunge kuanza kuchangia mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012, Hotuba za Bajeti ya Kambi ya
Upinzani Bungeni na ile ya maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi zimeungana kuikosoa, hasa katika eneo la ukuaji wa uchumi kushindwa kuondoa umaskini kwa Watanzania.
Hotuba hizo mbili zimeonya juu ya matumizi makubwa yasiyo na tija, ufisadi, matumizi mabovu ya rasilimali za nchi na misamaha mikubwa ya kodi kwa wawekezaji.
Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, iliyosomwa na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Bw. Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini- CHADEMA), imeenda mbali na kutoa mapendekezo na fomula ya kuongeza kima cha chini ya mshahara, kuweka utaratibu wa pensheni kwa wazee wote nchini, kupunguza kodi ya PAYE kwa wafanyakazi.
Katika kuhakikisha mapato yanaongezeka pia wamependekeza, kuwepo kwa utaratibu wa wapangishaji nyumba kulipa kodi kutokana na kiasi kikubwa wanacholipwa na wapangaji, wakati mwingine wakipangisha kwa malipo ya dola za Marekani.
Pia mbali na kubana kampuni kubwa kulipa kodi inavyostahili, imetoa maoni ya kufutwa kabisa kwa msamaha wa kodi kwenye mafuta kwa kampuni za madini na zile za ujenzi, kwani unasababisha upotevu mkubwa fedha za umma.
Pia kambi hiyo, kwa kutumia bajeti ya trilioni 14.160, italifanyia kazi na kulifufua Shirika la Ndege (ATCL), ambapo Mashirika ya Umma kama Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA) na TANAPA. Pia kufumua mfumo unaoruhusu posho za vikao, elimu ya bure kwa kuondoa ada za shule za sekondari na kupiga mnada magari ya anasa ya serikali yalipo sasa.
Akisoma hotuba hiyo jana, Bw. Kabwe alisema kuwa uchambuzi wao kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) unaonesha kuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi ni matumizi mabaya ya fedha za
umma, ambapo kwa mwaka wa fedha 2009/10 pekee, jumla ya sh. trilioni 2.4, sawa na asilimia 25 ya bajeti yote, zilitumika vibaya kwa 'na kulambwa katika mifuko ya wezi, wabadhirifu.'
"Sasa tumeanza kusikia vilio kutoka sekta binafsi kwamba na wao wapate unafuu huu wa kodi. Kambi ya Upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao uondoke katika utumishi wa umma. Ninaomba ieleweke kuwa hatupingi posho za kujikimu ambazo
viongozi au maafisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi.
"Posho hizo zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa. Lakini posho za vikao zifutwe mara moja. Ili kuonesha kuwa viongozi wa kisiasa tunaelewa kilio cha wananchi kuhusiana na gharama za maisha na kupunguza matumizi ya serikali, waheshimiwa wabunge tunaanza na posho za vikao vya bunge...polisi halipwi posho kwa kulinda, mwalimu halipwi posho kwa kuingia darasani na wala nesi halipwi kwa kusafisha vidonda vya wagonjwa...
Bw. Zitto alisema kuwa Kambi ya Upinzani inashauri kufanyika marekebisho katika mfumo wa posho na mfumo wa mishahara kwa watumishi wa umma, kwa kuanzia katika mjadala wa bajeti inayojadiliwa sasa, ili kurejesha imani ya umma kwa wanasiasa na
viongozi wao.
Katika bajeti yao, Kambi ya Upinzani Bungeni wamesema kuwa kiwango cha misamaha nchini ni kikubwa, ambapo kama ingetolewa katika kiwango cha misamaha ya kodi inayotolewa Kenya, kiasi cha sh. bilioni 484 zingeokolewa mwaka fedha 2008/09 na mwaka 2009/10 sh. bilioni 302, hivyo ikapendekeza kupitiwa upya vivutio vinavyotolewa na TIC kwa wawekezaji kwa kupiga marufuku msamaha wowote wa kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
"Katika sekta ya madini na makampuni ya kimataifa...tumeonesha katika tathimini ya uchumi namna ambavyo sekta ya madini imekuwa haichangii mapato ya ndani. Katika mwaka huu wa fedha taifa letu litakusanya sh. bilioni 99.5 kutoka katika mrabaha kwenye madini yanayochimbwa nchini kwetu. Mapato haya ya mrabaha kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia 4.5 tu ya mauzo ya dhahabu peke yake nje ya nchi.
"Kwa upande wa kodi nyingine zinazokusanywa kutoka katika sekta ya madini inakuwa ni vigumu kujua ni kiasi gani tunakusanya kwani kampuni zote zinalundikwa katika kapu moja la Idara ya Walipa Kodi Wakubwa. Kwa takwimu za mwaka 2009/10 mapato yote ya kodi pamoja na mrabaha na malipo kwa mifuko ya Pensheni (ambayo si kodi) katika sekta ya madini yalikuwa takribani sh. bilioni 256 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 16 ya thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi."
Katia kuhakikisha taifa linanufaika na sekta ya madini, Bw. Zitto alibainisha mbinu za kampuni kubwa za kimataifa, kamazile zinazohusika na madini na mawasiliano hapa nchini, kwa ajili ya kukwepa kodi kwenye nchi zinazoendelea, ambapo mara nyingi
hutumia sehemu kubwa ya uwekezaji wao kama mkopo.
Njia hiyo kwa mujibu wa Bw. Zitto, huwezesha wawekezaji wenye hisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji, kwa sababu wakati wa kukokotoa kodi wanayopasawa kulipa, riba huondolewa kwanza, hivyo kwa sababu tayari fedha nyingi zinakuwa tayari
zimepelekwa katika kulipa madeni, kampuni hizo huonekana zimepata hasara karibu kila mwaka.
"Katika kipindi cha miaka 2001-2009 kiwango cha kodi ambacho kingelipwa serikalini iwapo kampuni za madini zingewekeza mtaji wa angalau asilimia 30 za uwekezaji kwenye migodi yao kingelikuwa takriban dola za Marekani sh. mil. 830...sehemu kubwa ya fedha
zinazotokana na faida wanayopata kwenye mauzo ya dhahabu huishia kulipia madeni na riba, hivyo kukosesha serikali mapato. Muundo wa mitaji ya uwekezaji itapelekea makampuni haya kutangaza hasara kila mwaka."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Dkt. Abdallah Kigoda alikosoa utaratibu wa serikali kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji, akisema kuwa kamati hiyo inaamini suala hilo halitasaidia kuongeza wawekezaji nchini.
Alisema uwekezaji nchini utaongezeka kwa kuondolewa vikwazo vikubwa ambavyo ni rushwa, urasimu na ubinafsi, pia kuboresha miundombinu-barabara, reli, umeme, maji, kisha kuwa na sheria na taratibu zinazotabirika na endelevu, akiongeza kuwa utaratibu
wa Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unapasawa kuanza haraka, kwani fedha za sekta binafsi zitakuwa na mchango mkubwa hasa uwekezaji wa miundombinu.
"Kamati inarudia kuishauri serikali kudhibiti eneo la mapato na matumizi. Eneo hili bado ni changamoto. Matumizi ya serikali bado yanaendelea kuwa makubwa kuliko mapato. Mwaka 2009/10 mapato ya ndani ya serikali yalikuwa sh. 3,490.3 milioni na matumizi yalikuwa sh. 6,143.9 milioni. Kwa kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011 mapato ya serikali yalifikia sh. 4,256.3 bilioni na matumizi yalikuwa sh. 7,169.3 bilioni.
"Katika kipindi cha 2011-2012 mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa sh. 6,775.2 bilioni wakati matumizi ya kawaida ni sh. 8,600.3 bilioni. Mfumo wetu wa kibajeti unaonesha kuwa wa matumizi zaidi badala ya kuzalisha," alisema Dkt. Kigoda.
Kamati hiyo pia ilishauri kubanwa kwa wawekezaji wakubwa wa madini ili wachangie katika pato la taifa kadri ya faida wanayopata, pia wawekezaji hao wasaidie kuhifadhi mazingira na kuwezesha programu za miradi ya maendeleo kwenye maeneo ya
migodi.
"Pamoja na kuwa uchumi mkubwa umeendelea kufanya vizuri pamoja na changamoto za uhaba wa umeme, ukosefu wa mvua na matatizo mengine ya ki-miundombinu, serikali inatakiwa ibuni na iweke hatua ya kutafsiri mafanikio hayo na jinsi ya kuwagusa wananchi walio wengi vijijini ambao wengi ni maskini.
"Kwanza kuharakisha maendeleo ya kilimo, pili kujenga uwezo na ujuzi wa maskini, tatu ni lazima kuondoa vipingamizi na vikwazo katika shughuli ndogondogo wanazofanya maskini pamoja na shughuli za kijasiriamali, nne ni usawa wa kijinsia kwa fursa za uchumi na tano lazima sera na mipango yetu itengeneze fursa za ajira," alisema Dkt. Kigoda.
NASHAURI SERIKALI KUTHAMINI MAONI YENYE MASILAHI KWA TAIFA NA KUWEKA KATIKA BAJETI, "MIPANGO MEMA ILIYO KWENYE BAJETI YA SERIKALI + MIPANGO MEMA TOKA BAJETI KIVULI + MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA FEDHA NA UCHUMI" Tutapata bajeti itakayomkomboa mwananchi na kulivusha taifa kufikia malengo ya milenia 2025. NB:TUNAJENGA TAIFA MOJA
ReplyDeleteMUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA
Bila kuwapumzisha hawa mafisadi wa sisiemu hatuendi mahali, bunge livunjwe mara moja na uchaguzi huru ufanyike hapo ndipo mambo yataenda vinginevyo hamna kitu kitafanikiwa ndani ya taifa hili
ReplyDeletena hiyo katiba wanavuta tu hadi miaka iende,katiba ivunjwe,kuwe na serikali ya mseto kama kenya na zanzibar,mawazo ya wapinzani yaingie serikalini.bajeti ndio hiyo,wasifikiri wana jipya ccm,wajue watu vinjwa.nchi ina wasomi.siyo wao wanarignisha ufisadi tu na kula pesa za mikataba.chadema ndiyo hiyo,na bajeti ndo hiyo,ifanye kazi.
ReplyDeleteOle wenu msiosikia, msioona wala kunusu harufu ya kile kinachotokea Bara la Arabia!!.CCM na kiburi chenu, muda wenu umekwisha. Huu ndiyo mwisho wa sherehe mliyokuwa nayo tangia miaka hamsini!! Tanganyika itajivua tu gamba hili la CCM.Hii ni bajeti ya Chama Tawala na siyo ya Wananchi.
ReplyDeletePosho hizo si halali hata kama serikali inaendelea kuzing'angania eti sheria inaruhusu.Sheria hutungwa na kubadilishwa kwa kuzingatia nyakati na umhimu wa sheria hiyo kwa wakati mwafaka.Wakati huu posho hizi zinaonekana ni mzigo kwa mlipa kodi bali ni sherehe kwa baadhi ya wabunge kwani wanalipwa mara mbili kwa shughuli hiyo hiyo.Tazama,Mbunge analipwa mshahara,posho ya kutokuwepo kituoni kwake.Hii posho ya kikao analipwa kwa vigezo gani?Je kuhudhuria vikao vya bunge si sehemu ya kazi yake?Kama posho hizo zinakubalika kwa wabunge basi hata walimu wanapoingia darasani kufundisha wapewe posho za kufunndisha.Ni kweli kuna muda walimu walipewa "teaching allowance".Kwa nini zilifutwa na za wabunge kubakizwa kwa kuhudhuria kikao cha bunge?
ReplyDeletechadema wanafki watupu ,kwanini hawajashirikisha vyama vikongwe kama CUF kuandaa bugjet mbadala au tuseme wamelewa sifa za kupata wabunge wa kuchaguliwa tena wachache?
ReplyDeletehuu ni wakati wa serikali kupima mambo kwa uzito wake,badala ya kupima hoja kwa kuangalia inatoka upande wa kambi ipi ya upinzani.hivi hili la kutumia kuliko unachozalisha/kipata linahitaji waziri muhusika kuwa na PhD?Ni wakati wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa faida ya nchi,hii yenye raslimali nyingi lakini maskini ya kutupwa.
ReplyDelete