16 June 2011

SMZ yatanganza neema kwa wananchi

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza neema kwa wananchi wake kwa kutopandisha kodi yoyote katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12.Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Bw. Omar Yussuf Mzee, alipokuwa akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 katika kikao cha baraza la wawakilishi.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2011/2012 serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote badala yake itaimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo.

Alisema chini ya mfumo huo serikali itaziba mianya inayotumika kukwepa au kupunguza kodi na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuona kuwa kabla ya kuongeza kodi juhudi zinachukuliwa kwanza katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uwajibikaji.

waziri huyo alisema serikali itasimamia walipaji kodi kwenye vyanzo vilivyopo na kuhakikisha misamaha inayotolewa inatumika kwa dhamira iliyokusudiwa.

Alisema katika juhudi nyengine za kuongeza na kuimarisha mapato SMZ katika mwaka ujao wa fedha itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za Muungano wanaofanyakazi Zanzibar.

“Hatua hii imekuja kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya SMZ na SMT katika juhudi za kushughulikia kero za Muungano,” alisema waziri huyo.

Kuhusu suala la mishahara waziri huyo alisema serikali tayari imeshafanya mapitio na kuandaa mapendekezo mapya ya mishahara ya watumishi wa umma ambayo itaanza kutumika katika mwaka huu wa fedha.

Alisema viwango hivyo vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Alisema mapendekezo hayo ya mishahara mipya yamezingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu aliyonayo mtumishi, uzoefu na muda aliofanya kazi.

“Miundo ya Utumishi (Scheme) imewapa watumishi na nyongeza zao za mishahara kwa kuzingatia muda wa uajiri na kiwango cha elimu”, alisisitiza.

Alisema mbali na hatua hizo zinazochukuliwa serikali itakuwa ikiongeza maslahi ya watumishi wa umma kila mwaka pale hali ya uchumi na mapato ya serikali itakapokuwa nzuri.

Serikali ya Zanzibar katika mwaka wa fedha 2011/2012 inatarajia kutumia shilingi bilioni 613.08.

Kati ya fedha hizo mapato ya ndani yanakadiriwa kufikia sh. bilioni 221.24 wakati ruzuku pamoja na mikopo kutokana na misaada ya wahisani wa maendeleo ni sh. bilioni 340.96.

Alisema bajeti ya mwaka huu ni mwendelezo wa jitihada za Serikali ya Umoja wa kitaifa katika kufikia maendeleo ya Mpango wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA), malengo ya maendeleo ya Milenia na hatimaye dira ya maendeleo ya 2020.

Hata hivyo alisema ili kufikia malengo yao mapema zaidi kila mwananchi anapaswa kuwajibika na kushiriki kikamilifu kwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa kuzalisha mali na kujiongezea kipato, kwani ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment