*Kambi ya Upinzani yasema imejaa upotoshaji
Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Waziri Wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo kusoma makadirio ya mapato na matumizi ya serikali mbele ya bunge, Kambi ya
Upinzani Bungeni, imetoa tamko ikidai kuwa hotuba ya waziri huyo ilikuwa na upotoshaji wa kitakwimu na maudhui, huku pia ongezeko lake likiwa ni 'hewa', hivyo imeutaka umma wa Watanzania kutokubali kurubuniwa wala kupumbazwa.
Kambi hiyo kupitia kwa Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Bw. Zitto Kabwe imesema kuwa imeshtushwa na upotoshaji uliofanywa na serikali ya CCM kupitia kwa Waziri Mkulo, kwa lengo la kuwajengea wananchi matumaini hewa kuwa watapata nafuu ya maisha kupitia bajeti hiyo wakati hali halisi si hivyo.
Bw. Kabwe alijinasibu kuwa katika kuonesha kuwa bajeti ya serikali haiwezi kuinua uchumi wa watu wengi wa chini, Kambi ya Upinzani itawasilisha bungeni bajeti mbadala Jumatano, Juni 15, mwaka huu saa tano asubuhi, ambayo itakuwa 'inajali maslahi ya Watanzania, yenye lengo la kukuza uchumi wa vijijini, ikijikita katika kupata vyanzo vipya vya mapato na kubana matumizi ikiwemo posho mbalimbali'.
Huku akionesha mifano ya upotoshaji aliodai kuwa ni mkubwa, kitakwimu na kimaudhui, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Bw. Kabwe alisema kuwa ongezeko la bajeti linalosemwa kuwepo katika bajeti ya mwaka huu ni 'hewa', kwani ukweli ni kuwa hakuna ongezeko halisi lililofanyika na sehemu kubwa ya fedha zilizoongezeka zitalipia deni la taifa, hivyo kuifanya iwe 'bajeti ya madeni, si ya maendeleo'.
Alisema kuwa bajeti iliyopita ilikuwa sh. trilioni 11.6 na mwaka huu ni trilioni 13.525, ambapo katika fedha hizo, kiasi cha trilioni 1.901 sawa na asilimia 14.06 ya bajeti yote, kitatumika kulipa deni la taifa, hivyo mantiki inaonesha kuwa fedha za kuendeshea serikali na gharama za maendeleo zitabakia trilioni 11.624 ambazo ni karibu sawa na bajeti ya 2010/2011. Ingawa pia thamani ya shilingi imeshuka kulinganisha na ilivyokuwa mwaka wa fedha unaoisha.
"Wakati waziri akitaja kuwa kipaumbele cha kwanza cha bajeti hiyo ni kumaliza tatizo la umeme na hivyo kutamka kwamba ametenga sh. 537 bilioni, upembuzi uliofanywa na Kambi ya Upinzani kwenye vitabu vya bajeti vilivyotolewa na serikali yenyewe umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa jumla ya kiasi cha sh. 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi ya kawaida sh 76,953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya maendeleo zimetengwa sh. 325,448,137,000...(fedha hizo za maendeleo) zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa megawati 160, (100 Dar es Salaam na 60 Mwanza).
"Hakuna mradi wowote mpya wa umeme unaoonekana katika bajeti. Ni dhahiri kuwa kauli ya Mkulo ililenga zaidi kuwajengea wananchi matumaini hewa kuliko kuchukua hatua za ukweli kumaliza tatizo la umeme," alisema Bw. Kabwe.
Aliongeza: "Wakati waziri akisema bungeni kuwa bajeti ya mwaka 2011/2012 itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kudhibiti matumizi (uk. 53 wa hotuba), ukweli ni kuwa bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012 imetenga jumla ya sh. 0.987 trilioni sawa na asilimia 13 ya bajeti, kulipia posho.
Taarifa hiyo ya Bw. Kabwe pia iliongeza kuwa maeneo mengine ambayo ilidai serikali kupitia kwa Bw. Mkulo ilipotosha umma kwa makusudi, ni katika udhati wa kauli ya kupunguza posho, kwani wakati waziri akisema hivyo katika hotuba, bado alipendekeza kwa bunge kurekebishwa kwa Sheria ya Kodi ya Mapato sura ya 332 ili pamoja na masuala mengine, kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka bajeti ya serikali.
Pia alisema kuwa bajeti ya serikali mwaka mpya wa fedha, imewaongezea mzigo mkubwa wananchi, hasa wajasiriamali wadogo na vijana ambao wamejiajiri ama kuajiriwa kwenye biashara ya usafiri na usafirishaji, kwa kufanya marekebisho katika sheria ya usalama barabarani sura ya 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati mtu akiendesha gari, kutoka sh. 20,000 mpaka sh. 300,000.
"Lakini wakati Waziri Mkulo katika hotuba yake aliyoitoa jana ukurasa wa 74 alitamka kuwa wataongeza kiwango cha faini (kutoka 20,000) hadi kufikia sh 50,000...ni dhahiri kuwa kauli ya waziri ya kusema faini itafikia 50,000 wakati kwenye vitabu rasmi vya bajeti faini hiyo inaonekana itafikia 300,000, hivyo alilenga kuuhadaa umma na kuupotosha," alisema Bw. Kabwe katika taarifa yake hiyo.
Aliongeza kuwa Kambi ya Upinzani Bungeni imestushwa na kushangazwa na hatua ya serikali kutenga zaidi ya robo ya bajeti (asilimia 27) kulipa madeni na posho, ambapo asilimia 14 italipa madeni na 13 italipa posho mbalimbali.
Utegemezi wa bajeti
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HAKIARDHI, Bw. Yefred Myenzi alisema kuwa bajeti bado inaendelea kuwa tegemezi, kwani sehemu kubwa inategemea fedha kutoka kwa wafadhili.
Alisema kuwa fedha nyingi ambazo zimeelekezwa kwa ajili ya matumizi ya serikali, ambayo ni makusanyo ya ndani yagawanywe nusu yapelekwe katika matumizi ya kimaendeleo badala ya kutegemea fedha za wafadhili katika shughuli za maendeleo ambazo huwa hazifiki kwa wakati.
"Sioni kama bajeti hii inachochea uzalishaji katika kilimo, sekta ya wazalishaji wadogo wadogo na wafugaji, kinachotakiwa ni watu hawa kupatiwa nyenzo za uzalishaji na siyo kupewa Power Tiler kutoka China, kwani hazikidhi mahitaji ya wakulima wadogo, serikali iwapatie ruzuku na mbolea," alisema.
Alisema kuwa wadogowadogo hawatanufaika kwa chochote na bajeti hiyo ya kilimo, bali wakulima wakubwa ndio pekee watakaonufaika.
Kauli ya wanasiasa
Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Dkt. Paul Kyara alisema kuwa bajeti hiyo ni nzuri lakini kinachotakiwa ni utekelezaji na siyo maneno.
Alisema kuwa ajira ni bomu ambalo lilikuwa linasubiri kulipuka, lakini Waziri Mkulo amelizingumzia vizuri na kama litasimamiwa ipasavyo vijana watafaidika.
Naye Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa bajeti hiyo haitamkomboa Mtanzania kwa sababu kuna sekta nyeti ambazo hazijazungumziwa kama madini, ambayo waziri hakuzungumzia yanachangia vipi pato taifa.
"Sekta ya madini ndiyo yenye mchango mkubwa wa taifa lakini tunaona waziri hakuzungumzia lolote katika bajeti hii, nasisitiza kwamba bajeti hii haina kitu,"alisema.
Prof. Lipumba alitaka kuwepo kwa utekelezaji wa bajeti hiyo na isiwe kiini macho kwa Watanzania na kuongeza kwamba Waziri ameshindwa kuainisha vitu na kuelezea vimepunguzwaje.
Wasiwasi wa wafanyakazi
Wafanyakazi nchini wameonyesha wasiwasi mkubwa ikiwa ni pamoja na kuiponda bajeti hiyo walichotegemea ni kupandishwa kwa mishahara lakini Waziri Mkulo hakuzungumzia kupandisha wala kusudio la serikali la kupandisha mishahara.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Bw. Nicholaus Mgaya, alisema ameshangazwa na bajeti hiyo, kwani wamekuwa wakikutana na serikali kuhusu maslahi ya wafanyakazi lakini bajeti imewapiga chenga.
"Kwa kuwa siyo mwisho wa bajeti, tutakaa tuone ni jinsi gani mishahara itapandishwa kwani Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Bi. Hawa Ghasia hajatoa bajeti yake," alisema Bw. Mgaya.
Alisema alishangazwa na hotuba ya bajeti hiyo kwani Bw. Mkulo alichokuwa akikisisitiza ni kwamba ataboresha maisha ya wafanyakazi wa sekta ya umma na ile ya binafsi lakini alidai sicho walichotegemea wafanyakazi.
Wafurahia fungu la kilimo
Bajeti ya kilimo ya sh bilioni 926.2 imewafurahisha baadhi ya wananchi, wakisema zitasaidia kuboresha miundombinu na kuwafikishia pembejeo wakulima katika kila kaya.
"Bajeti ni nzuri, lakini kuna tatizo moja kwamba hawa wameidhinisha mabilioni ya fedha kwa ajili ya kilimo, je, ni kweli watendaji hasa maafisa kilimo na wataalamu wa pembejeo wataweza kuzitumia vilivyo au ubadirifu utakuwepo hivyo kukwamisha jitihada zetu," alisema Bw. Mershark Moshi mfanyabiashara katika soko la Kariakoo.
Bw. Said Said Nembo mkazi wa Ilala alisema kuwa kupitia fedha zilizoelekezwa katika sekta ya kilimo zitasaidia kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ikiwa na kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kupata pembejeo na zana bora za kilimo.
Wakati huo huo wananchi wengine wamesema kuwa serikali haikutendea haki kuzitoza bidhaa ambazo siyo za lazima kodi ndogo kama vile sigara na pombe kwa kuwa bidhaa hizo zilipaswa kupanda zaidi.
"Wangepandisha ushuru zaidi katika bidhaa zile ambazo hazina ulazima wa kuwepo kwa ajili ya mahitaji ya kila siku, mfano sigara iuzwe sh. 1,000 kila moja na pombe ikiwezekana ziuzwe kwa sh. 5,000 halafu faida hizo zitumike katika kufidia unga, sukari na vyakula vingine," alisema Bw. Marko Mwakipembe mkazi wa Mbagala Zakhiem.
Vyanzo vipya vya kodi
Serikali imetakiwa kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuondoa suala la leseni za biashara kama chanzo cha mapato kwani kuweka chanzo hicho ni kuwachanganya wafanyabiashara.
Katika bajati ya mwaka huu imerudisha chanzo cha mapato cha leseni za biashara hali ambayo imelalamikiwa na wadau mbalimbali waliochangia bajeti hiyo na kutoa maoni yao juu ya viashiria mbalimbali vya bajeti.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Ester Mkwizu aliesma kuwa serikali inatakiwa kutambua fursa zilizopo za kukusanya mapato na si kuwakandamiza wafanyabiashara kwa kuwarudishia kodi ya leseni ambayo serikali iliiondoa mwaka 2004.
Mwaka 2004 serikali iliondoa kodi hiyo kwa lengo la kuwapunguzia wafanyabiashara gharama za uendeshaji katika biashara lakini cha kushangaza
ni kuona serikali inarudisha kodi hiyo ya leseni kwa wafanyabishara ambayo ni kikwazo kwao kwan inawapa ugumu.
Aliishauri serikali kuhakikisha kuwa inakusanya kodi kwa kuiongezea wafanyakazi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuweka vifaa muhimu vya kuwawezesha kukusanya kodi kikamilifu.
Bi. Mkwizu alisema anaamini kuwa kuna mapato mengi ambayo
hayakusanywi, na kama sheria sheria hiyo haisimamiwa kwa umakini watu wengi wataendelea kutojisajili kwenye vyombo vya kibishara ambako wengi wangelipa kodi.
Imeandaliwa na Godfrey Ismaely, Dunstan Bahai, Gladness Mboma na Grace Michael, Dar; na Pendo Mtibuche na Tumaini Makene, Dodoma
hakuna mtu wa kushangaa hilo tunalijua sababu alikuwa tayari kapata kitu kichwani tunajua hakuna jambo lolote jema litakalo fanywa na serikali hasa kwa chadema ambao macho yemewatoka wakiwania ikulu ambayo wataisikia tu redioni
ReplyDeletemaneno ya pombe haya tunayajua
ReplyDeletebajeti imejaa takwimu za uongo mtupu
ReplyDeletenilini Tanzania tutaendelea kwa mtindo huu wa kudanganya hata kwenye vitu muhimu kama bajeti.
ReplyDeleteBajeti kila mwaka inafikiria kuongeza bei ya bia na sigara tu,kama trend itaendelea hivi 2015 bia itakuwa shs 5000.Nadhani bajeti hii ita encourage magendo ya bia toka kenya na zile nile special za Uganda kwani sasa zitakuwa cheap compared to bia za Tanzania,Note: Uwezi kupiga vita unywaji wagongo wakati unapandisha bei ya bia,people will continue to opt for the cheapest.
ReplyDeleteNadhani hii ni danganya toto ambayo tunatakiwa kuwa makin sana watanzania ili tuweze kupiga hatua katika maisha yetu ya kila siku..........
ReplyDeleteTunataka Mkulo atwambie specifically posho ambazo hazina TIJA alizoziondoa ni zipi? Halafu kwa kuondoa hizo posho zisizo na TIJA serikali itakuwa imeokoa shilingi ngapi? Bila kufanya hivyo itakuwa ni UCHAKACHUAJI tu.
ReplyDeletePia tunaomba Mkulo utueleze specifically kodi alizopunguza kwenye bidhaa ya mafuta (disel, and petrol) ni zipi? na zimepungua kwa kiasi gani? Na kutokana na punguzo hilo serikari itakosa mapato ya sh ngapi? Mbona ailpopandisha kodi za pombe, sigara, vinywaji baridi alitoa figures? Kwanini kwenye mafuta hakufanya hivyo kama sio chnaga la macho?
CCM sasa munaipeleka nchi kubaya, kama hata kwenye budget mmefikia KUCHAKACHUA, hii haiwezi kuvumilika.
naomba Mbunge wa Arusha mjini arudie lile swali lake bungeni juu ya atumie kipengele kipi kumshitaki kiongozi kama waziri wa fedha anapolidanga bunge na wananchi kwa ujumla hasa kwa kutoa takwimu za uongo mkubwa namna hii? pengine Makinda anaweza akampa jibu sahihi.
ReplyDeleteWezi hao
ReplyDeleteHata wangesema vipi mmekalia kupinga kila kitu ili kupotosha umma.mlaaniwe ili mshindwe Wa Tanzania wamewachoka.Bajeti imetolewa ili ijadiliwe na hao wawakilishi wenu na kuiboresha isingekuwa rahisi kubuni mnacho taka kwenye bajeti kinacho onekana hapa hamujui maana ya bajeti,wajibu wa serikali,wajibu wa Raia.Hatachama kingine kikishika madaraka matabaka yatakuwepo cha msingi tuungane na kusimamia pesa zetu na kukabiliana na wizi Serikalini.
ReplyDeleteNdugu Watanzania napenda kutoa maoni yangu kuhusu mpango wa makadirio ya BAJETI kwa kufatilia maendeleo yanayotakiwa nchini.
ReplyDeleteKwanza inapaswa kujadiliwa BUNGENI kuhusu maendeleo yanayotakiwa kufanyika katika nchi na kufatia kila mkoa mahitaji yake. Baada ya kukubaliana BUNGENI kwa maendeleo yanayo hitajika kutekelezwa kwa kutumia kura za wengi Bungeni ndiyo iandikwe hiyo orodha ya maendeleo. Hapo ndipo itabainika ugawaji sawa wa maendeleo kwa kila mkoa na haitatokea malalamiko yoyote kuhusu ugawaji wa BAJETI kwa wananchi wote na itakuwa imekubalika kwa kila Mtanzania.
Sasa Tanzania tunapiga hatua maana kwakweli wananchi wote wenye aliki na vichaa tunashiriki moja kwa moja katika kuongoza nchi yetu. Kwani jana ktk mjadala wa Bajeti ktk kituo kimoja cha TV nilimuona mtu akishiriki ktk mjadala huo kwa kusema mimi sijui hii bajeti na kuishia HAPO na alishangiliwa SANA bila shaka na vichaa wenzake. Hongera kwa serikali kwa kuturuhusu kuongea.
ReplyDeletewe msemaji hapo juu, tuisikitikie serikali kwa kutoweka mazingira bora ya ustawi wa jamii ya watanzania. hao sio vichaa ila wamekosa elimu bora yenye kuwafanya waweze hata kujieleza kwenye TV. wewe pia unaoneka unatatizo hilo.
ReplyDelete