09 June 2011

Bajeti sikivu

Tumaini Makene na Pendo Mtibuche, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkullo amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka 2011/2012, bungeni ambayo kwa kwa ujumla
yameonekana kuwa ni bajeti sikivu, kwa kuzungumzia masuala tata ambayo yamekuwa yakielezwa kuwa chanzo cha ukali wa maisha na kuongeza umaskini wa Mtanzania.

Kwa uhalisia na maoni ya watu mbalimbali, bajeti hiyo imeonekana kushusha munkari ya wananchi juu ya hali ngumu ya maisha, na madai ambayo yamekuwa yakipigiwa 'vuvuzela' na vyama vya upinzani kama kipimo cha utendaji wa serikali ya Chama cha Mapinzudi.

Masuala hayo ambayo kwa muda mrefu sasa yamekuwa yakipigiwa kelele na wananchi wengi, vyama vya siasa vya upinzani, asasi za kiraia zisizokuwa za kiserikali pamoja na viongozi kadhaa wa serikali ni pamoja na kupanda kwa bei ya za bidhaa na huduma na ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana.

Bw. Mkulo akiwasilisha bajeti hiyo jana bungeni Dodoma alisema kuwa maeneo hayo na sababu zake kama vile ongezeko la bei za mafuta, upungufu wa nishati ya umeme, upungufu wa chakula yatawekewa mkazo katika kutafutiwa ufumbuzi kwa nia ya kumpatia mwananchi unafuu wa maisha na kuwateletea maendeleo Watanzania kwa ujumla.

Akisoma bajeti hiyo ambayo pamoja na kutoa ahadi ya kushughulikia tatizo la ukali wa maisha, bado imeendelea kukwepa suala la kuongeza wigo wa utozaji kodi hasa katika kupata mapato ya kutosha kutoka katika utajiri wa rasilimali madini ambayo Tanzania imebarikiwa kuwa nayo, Bw. Mkullo alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali inatarajia kutumia jumla ya sh. trilioni 13.5.

Mgawanyo wa fedha hizo utakwenda kulingana na vipaumbele vya taifa, kama ifuatavyo:

Miundombinu:     Trilioni 3.7/-
Umeme:        Bilioni 539.3/-
Maji:        Bilioni 621/-
Kilimo:        Bilioni 926.2/-
Elimu:        Trilioni 2.2/-
Afya:        Trilioni 1.2/-


Kwa mujibu wa Bw. Mkullo Serikali inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya sh. bilioni 6,775.9 sawa na asilimia 17.2 ya pato la taifa, ambapo mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa sh. bilioni 350.5. Serikali inategemea kukopa kiasi cha sh. bilioni 2,475.9 kutoka ndani na nje.

Wakati washirika wa maendeleo watasaidia kupitia misaada na mikopo kwa jumla ya sh. bilioni 3,923.6, serikali inatarajia kutumia jumla ya sh. bilioni 8,600.3 kwa matumizi ya kawaida, huku ikitumia sh.
bilioni 4,925.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Hata hivyo, Majira lilifanikiwa kupata vitabu vya bajeti hiyo ambapo kwa mfano wakati Bw. Mkulo alisema kuwa posho zimeondolewa, bado vitabu vinaonesha mambo tofauti.

Pia pamoja na kuzungumzia kupunguza tozo katika bidhaa za mafuta, hakuainisha ni jinsi gani tozo hiyo itapunguza bei ya mafuta kwa kuwa kinachoongeza bei si tozo, wala EWURA, SUMATRA, bali kodi ya bidhaa hiyo.

Katika bajeti hiyo serikali imeweka mikakati yake kupunguza msongamano wa magani na makosa ya barabarani ambapo kiwango cha fani kimepandishwa kutoka sh 20,000 hadi sh 200,000.

Wapinzani walia na umeme

Baadhi ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wametoa maoni yao juu ya bajeti na kuitaka serikali iache propaganda katika kutenga fedha za kuinua sekta ya umeme.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya Bw. Mkulo kuhitimisha  kusoma bajeti ya serikali, Mbunge wa Ubungo, (CHADEMA), Bw. John Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alisema kuwa kwa sasa nchi inakabiliwa na upungufu wa umeme unaofikia
megawati 260 na utaendelea kuongezeka kila mwaka endapo serikali itaendelea na poropaganda katika kushughulikia sekta ya umeme.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe alisema  umeme ni suala lililopewa kipaumbele katika bajeti hiyo lakini fedha zilizotengwa ni kidogo, hivyo wao kama upinzani watatoka na bajeti yao mbadala ambayo wataiwaisilisha Juni 16, mwaka huu na itaeleza hali halisi ya uhitaji wa fedha katika sekta hiyo.

4 comments:

  1. Mimi naona bajeti si mbaya saana hasa katika suala zima kupunguza ukubwa wa misafara ya viongozi pamoja na kuongeza kodi kwenye vileo na sigara vitu ambavyo havina manufaa yoyote katika mwili wa mwanadamu, kikubwa ni ufuatiliaji na utekelezaji wa malengo mazima ya hiyi bajeti.

    ReplyDelete
  2. Tusubiri ya wapinzani,tujue na upande mwingine wa shilingi uko vipi, maana kote wasomi hasa wachumi wapo,akili zote safari hii zimepanda juu,kila mtu anajua kilio cha wananchi ni mafuta na umeme.bila hivo hakuna ahueni hasa kwa sisi wakesha hoi na walipa kodi wakuu!

    ReplyDelete
  3. Hii bajeti haijaonyesha njia za kuzuia hizo safari za ndani na nje, labda kama serikali iseme ilikuwa inajitungia tu safari hata pale pasipohitajika, lakini kama safari zilikuwa za tija na zilikuwa zinaandaliwa na wadau bila shaka zitaendelea tu kuwepo. Mimi roho inaniuma kuona kauli zinazotolewa hazina mashiko, yaani hazielezi ni namna gani malengo hayo yatafikiwa. nadhani mwalimu na mwanafunzi mzuri ni yule anayekokotoa swali la hesabu/anayeonyesha formula badala ya kutoa jibu (pasipo kuonyesha kwa ufasaha jinsi alivyopata jibu). Kwa mtindo huu watanzania tutaendelea kuhubiriwa porojo zisizotekelezeka. Hapa ni vigumu kusema kupunguzwa kwa safari ni kwa asilimia, kwa nambari yaani kuwa safari zitakuwa 50 badala ya 100? zitachujwaje na watanzania tutajuaje kweli hizo safari hawakwenda na posho hazikulipwa?

    ReplyDelete
  4. SERIKALI MSIBABAISHW WATANZANIA KWANZA SEMENI VYANZO VIKUU VYA MAPATO YA TAIFA VINAINGIZA KIASI GANI KWA MWAKA ACHENI KUZUNGUKIA MIFUKO YA WALALA HOI WATANZANIA WAKATI NYINYI MNA PONDA RAHA MAHOTELINI MIEZI 7 KWA KUJINUFAISHA KWA HELA ZA WATRANZANIA WALIPA KODI, MMEZIDI NA WIZI WA KIMACHOMACHO WA KUWANYONYA WANYONGE WATANZANIA. TOWENI BAJETI YENYE KINA NA SI KUBABAISHA WATANZANIA WALIYO ZIBWA MIDOMO KWA KUOGOPA POLISI WENU WASIWAKAMATE NA KUWANYONGA KWA RISASI BILA HURUMA KAMA WAFANYAVYO SASA.

    ReplyDelete