18 May 2011

Wahandisi, washauri acheni kuoneana wivu-Magufuli

Na Grace Ndossa

WAHANDISI pamoja na Wataalamu Washauri wametakiwa kuacha kuoneana wivu badala yake washirikiane katika kufanya kazi, pamoja na kupeana
zabuni kwa lengo la kusaidia watalaamu wa ndani.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli kwenye uzinduzi wa leseni ya uhandisi, kuwa wahandisi wengi wanaoneana wivu na kushindwa kupeana kazi, hivyo wanatakiwa kuacha tabia hiyo na kushirikiana.

Alisema kuwa wanatakiwa kuacha tabia hiyo mara moja ili waweze kufanikiwa katika kazi pamoja na kushirikina na kampuni nyingine.

Pia aliitaka Bodi ya Wahandisi kuwadhibiti wahandisi wala rushwa, kitu ambacho alisema kinasababisha kutengenezwa kwa barabara chini ya viwango.

Aliongeza kuwa wahandisi ambao hawatekelezi kazi zao kwa wakati  wanatakiwa kufutwa ili wakavue samakini baharini.

Dkt. Magufuli alisema kuwa miradi mingi inayotelekezwa iko chini ya kiwango, hivyo wahandisi watii sheria kama wachungaji wanavyoshika amri kumi za Mungu.

Alitoa wito kwa bodi ya wahandisi kukagua barabara zote nchi nzima kuona kama zimekidhi viwango vya kutosha au la, hasa kwenye halmashauri ambako aliwataka wajue kama wahandisi waliopo wana ajira na wamesajiliwa kwenye bodi yao.

"Hii ina maana kwamba barabara zinazosimamiwa na halmashuri nyingi hazitumii wahandisi wanatafuta tu mtu wa kusimamia, hivyo mnatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka kupokea rushwa," alisema Dkt Magufuli.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Ninatubu Lema alikabidhi ripoti ya ukaguzi wa barabara ya Kilwa kwa Dkt. Magufuli kuhusu uchunguzi walioufanya.

Alisema kuwa bodi hiyo imebaini mapungufu mengi yaliyofanyika katika barabara ya Kilwa na si salama, hivyo wameishauri serikali kutazama upya miradi inayofadhiliwa na watu kutoka nje na kufuatilia kwa ukaribu.

No comments:

Post a Comment