Veronica Modest na Raphael Okello, Bunda.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Bw. Wilson Mukama amewatoa wananchi hofu akitamba kuwa CCM ni kama taasisi hivyo si rahisi kufa kama
wapinzani wanavyodai.
Alisema kuyumba kwa chama hicho kinatokana na changamoto nyingi zinazojitokeza katika vyama mbalimbali vya kisiasa duniani katika karne ya 21 na kwamba hiyo haijathibitisha kuwa CCM inakufa.
Akihutubia mamia ya wananchi na wanachama wa chama hicho katika Wilaya ya Bunda jana, alisema kutokana na changamoto hizo CCM imechukua hatua madhubuti ya kujipanga.
“Ni kweli tuko katika kipindi kigumu cha karne ya 21 ambacho chama chetu kinakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo tumeamua kujiangalia upya kukabili changamoto hizo,” alisema Bw. Mukama.
“Lakini CCM ni taasisi kubwa, taasisi ambayo imeshajiimarisha ikiwa na watumishi wengi wenye ujuzi katika siasa, kwa hiyo taasisi kama shule,hospitali na zinginezo haziwezi kufa kiurahisi kwa sababu kama kuna
watendaji wasiofaa huondolewa kazini na kuwaajiri wengine, hiyo ndio CCM,”
alisema.
Alibeza alichodai kauli ya wapinzani kuwa Rais Jakaya Kikwete hawezi kuongoza nchi hadi mwaka 2015 kwa madai kuwa nchi imemshinda na kusababisha maisha magumu kwa kupanda kwa gharama ya maisha.
Alieleza kuwa Rais Kikwete alichaguliwa kwa kura nyingi ya wananchi katika uchaguzi wa kidemokrasia, hivyo si rais kuondolewa katika nafasi hiyo kiurahisi mpaka muda wake utakapofika.
Pia alibeza kauli kuwa kujivua gamba kwa CCM haitasaidia chama hicho kujiimarisha kwa kuwa sumu ya nyoka ni ile ile hata akijivua gamba, akisema sumu ya CCM ni mbinu zake za kuendelea kushika dola.
Alifafanua kuwa baadhi ya watu wanatumia vibaya dhana ya CCM ya kupambana na wafanyabiashara mafisadi ndani ya chama hicho na kueleweka kuwa wafanyabiashara wote hawatakiwi kuwa wanachama au viongozi ndani ya chama hicho.
“Si kwamba CCM haiwataki wafanyabiashara wote kwa sababu ukifanya hivyo umekiua chama, tunachomaanisha ni wale wanaotumia fedha zao kuhujumu nchi,” alisema Bw. Mukama.
Kuhusu vyama vya siasa kuongozwa na wafanyabiashara, alikiponda Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kuwa waasisi wake ni wafanyabiashara
wakubwa ambao Hayati Mwalimu Nyerere alikataa sera zao wakati wa uhai wake.
No comments:
Post a Comment