26 May 2011

Vyombo vya dola vimeua watu 73

*Ripoti ya LHRC mwaka 2009/2010 yabainisha
*Polisi yaongoza uvunjaji haki za binadamu


Na Tumaini Makene

WAKATI sakata la mauaji katika Mgodi wa North Mara likiwa halijapoa, Jeshi la Polisi limezidi kuingia katika tuhuma za uvunjaji wa
haki za binadamu kwa kufanya mauaji kinyume cha sheria, Ripoti ya Haki za Binadamu nchini kwa mwaka 2010 imesema kuwa kwa mwaka huo pekee, vyombo vya dola vyenye wajibu katika kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi, vimeua wananchi 52.

Kutokana ripoti hiyo kubainisha suala la mauaji ya raia yanayofanya na polisi kuwa ni moja ya ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi uliofanywa mwaka uliopita, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho huandaa ripoti hiyo kila mwaka, Bw. Francis Kiwanga ametoa wito, 'polisi sasa waache kuwa vinara wa mauaji', akisema kuwa wanapaswa kuwa mfano bora wa kulinda sheria badala ya kuzivunja.

Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa kwa kufuata taratibu za utafiti wa kisayansi, kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama vile kuwahoji watu (5,000) kutoka wilaya 30, taarifa za vyombo vya habari na taarifa za wawakilishi wa LHRC walioko katika kila wilaya nchini, imesema kuwa vitendo vya mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia kinyume cha sheria vimeongezeka kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2009 ambapo watu 21 waliuawa, mpaka asilimia 72 (2010) ambapo watu 52 waliuawa.

Ikizungumzia sababu za mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola, ripoti hiyo imezitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa askari wenye utaalamu wa kutosha na maadili ya kazi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, mfumo dhaifu wa utoaji haki, uchunguzi wa matukio ya namna hiyo kufanywa na polisi wakati wao ni watuhumiwa, hivyo kutoa maamuzi au taarifa zinazoegemea upande mmoja na serikali 'kuwalinda' wale wanaohusika katika uvunjaji huo wa sheria na haki za binadamu, kwa kutochukua hatau stahili.

Ikitoa mifano ya ukiukwaji wa haki ya kuishi nchini kwa mwaka 2010, ripoti hiyo ambayo ilisomwa jana na Bw. Patience Mlowe, Bi. Haurus Mpatani na Bw. Onesmo Ulengurumwa, ilisema 'vyombo vya dola vinavyoongoza kwa mauaji ya raia kinyume cha sheria ni polisi, wanamgambo, askari magereza na walinzi wa kampuni binafsi za ulinzi. Utafiti wa LHRC unaonesha kuwa kati ya Januari hadi Desemba mwaka 2010, watu 52 walikufa wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

"Katika Mgodi wa North Mara polisi waliua watu 10 kati ya hao 52 waliouawa (mwaka 2010)...bado kuna vifo vingi vya namna hiyo vinatokea (maeneo mbalimbali) lakini havijapata nafasi ya kuripotiwa...chati yetu inaonesha kuwa mauaji haya yamekuwa yakiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka 2010 yameongezeka kwa kasi mno ikilinganishwa na mwaka 2008 na 2009," imesema sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza;

"Utafiti wetu juu ya mauaji katika Mgodi wa North Mara uliofanywa Juni, 2010 unaonesha kuwa takribani watu 19 wameuawa tangu mwaka 2009 hadi 2010.

"Pia tumebaini kuendelea kuwepo kwa matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuua watuhumiwa hasa katika maeneo ya miji mikubwa, Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kusini.

"Kati ya mwaka 2007 hadi 2010 jumla ya vituo nane vya polisi (Hedaru, Chato, Mbarika, Katoro, Kongowe, Makananga, Ilondele) vimevamiwa na makundi ya watu na vingine kuchomwa moto, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Mbali ya vyombo vya dola, ripoti hiyo pia imebainisha uvunjaji mwingine wa haki ya kuishi, ikisema, "Utafiti wa LHRC unaonesha kuwa haki ya kuishi imeendelewa kuvunjwa kwa namna mbalimbali kama vile kuendelea kuwepo kwa hukumu ya kifo ambapo mahakama zimeendelea kutoa hukumu hiyo. Pia mauaji ya imani za kishirikina, watu kujinyonga, uhalifu wa majumbani, watu kujichukulia sheria mkononi na kuua, na ajali za barabarani.

"Watu waliohojiwa wameeleza sababu ya kuendelea kuwepo kwa matukio ya watu kujichukulia sheria ni pamoja na ukosefu wa uelewa katika masuala ya sheria, ukosefu wa vituo vya kutosha vya polisi, watu kutokuwa na imani na jeshi hilo na serikali kutovipatia uzito stahili vitendo hivyo...mauaji ya kishirikina yameendelea kuwepo lakini jambo nzuri ni kuwa mauaji dhidi ya albino kwa mwaka 2010 hayakuwepo kabisa ingawa usalama wao bado haujawa imara kwani kuna matukio ya kuvamiwa na kutishiwa maisha yao."

Katika ripoti hiyo, Jeshi la Polisi pia ambalo pia limetuhumiwa kuongoza kwa kuvunja haki kwa kuwatesa raia wanapokuwa rumande, kiasi cha askari mmoja kuwahi kumchoma machoni sindano ya tindikali mmoja wa watuhumiwa, limetajwa kuwa ni taasisi inayoongoza kwa tuhuma za rushwa nchini, ikifuatiwa na mahakama.

Ripoti imesema kuwa katika taasisi zote za nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zilizofanyiwa utafiti kwa mujibuwa Ripoti ya Rushwa mwaka 2010, jeshi hilo limeshika nafasi ya tano likiwa na alama zipatazo asilimia 65.1.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mbunge wa Mhambwe (NCCR-Mageuzi). Bw. Felix Mkosamali ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa ripoti hiyo ambayo imezungumzia masala yote ya ukiukwaji wa hazi zote za binadamu nchini kwa mwaka 2010, inapaswa kufanyiwa kazi na kila mdau nchini, akisema kuwa mfumo wa utoaji haki nchini bado ni mfinyu hivyo mashirika kama LHRC yanahitajika kusaidia.

Alisema ni wakati mwafaka sasa wakati wa mjadala wa katiba mpya, Watanzania wahakikishe kuwa haki zote zikiwemo zile za kijamii na kiuchumi zinapata nafasi ili ziweze kudaiwa mahakamani iwapo itatokea zimeminywa katika mfumo wa utoaji haki nchini.

Mapema, Bw. Kiwanga alisema kuwa mwaka 2010 yameendelea kuwepo matukio yanayodhihirisha kuwa Tanzania bado inayumba katika utekelezaji wa kusimamia upatikanaji wa haki za binadamu, akitoa mfano kuwa wananchi wengi bado hawaridhishwi na utoaji wa haki kwa upande wa mahakama, hasa katika kuchelewa kusikilizwa na kuamuliwa.

Alisema pia kuna ongezeko la ukatili wa majumbani dhidi ya wanawake na watoto, yakiwemo kuc homwa moto, kukatwa mikono, kunyongwa, huku pia akilaani polisi kuendelea kujichukulia sheria mikononi kwa kuua au kujeruhi raia bila kufuata sheria, akisema 'polisi wasiwe vinara wa kuua, wanapouwa wanafundisha nini kwa jamii.

Alitoa madai mazito kuwa haki za binadamu nchini zinaendelea kuminywa wakati serikali imeshindwa kuteua au kuongeza muda wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambao karibu wote muda wao umeisha tangu Desemba mwaka jana. "Haki za binadamu zitaendelea kupotea na hakuna pa kukimbilia...tangu mwka jana hizi habari ni za uhakika makamishna wote wamemaliza muda wao na hakuna appointment wala aliyeongezwa muda na hawa ndiyo wanafanya kazi za tume," alisema Bw. Kiwanga.

Ahadi ya vijana CHADEMA

Naye Stella Aron anaripoti kuwa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamelaani mauaji ya wananchi wasio na hatia yaliyofanywa na polisi na kuahidi kuwa watahakikisha kuwa waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa wa Dar es Salaam, Bw. Henry Kilemo alisema kuwa vitendo hivyo vinafanywa kwa maslahi ya watu wachache na kusahahu kuwa wananchi wote wana mamlaka ya kudai kila wanachokiona si sahihi.

Alisema kuwa umoja huo unawapongeza makamanda wanaopigania haki na kuibuka na ushindi mkubwa kwa kuhakikisha haki inatendeka na Mtanzania anaheshimiwa katika taifa lake.

"Ni wazi kuwa jambo kama hilo la mauaji ya raia lilitokea Arusha, sasa Tarime na kesho wataua Dar na kutoa ubani, huu ni upuuzi na hatuwezi kuuvumilia kamwe," alisema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo mwenyekiti huyo amesema kuwa watahakikisha kuwa waliohusika na mauaji hayo wanachukuliwa hatua na kuwataka Watanzania kufahamu kuwa serikali iliyopo si ya kuwalinda bali kuwapora haki zao za msingi kwa maslahi ya watu wachache.

5 comments:

  1. Hichi kituo mbona hawajatoa takwimu kwa askari polisi waliouawa na wananchi kinyume cha sheria kwani wao sio binadamu au wao wanastahili kifo kisichohalali?Wawe wanasema yote sio upande mmoja tu.Polisi naye ni Binadamu

    ReplyDelete
  2. Hao wa haki za binadamu wangejua ugumu wa kazi ya polisi wasingesema wanaua watu,mbona hawatoi takwimu za raia waliouwawa na majambazi kwa mwaka 2010 au tuseme hao hawakuwa na haki ya kuishi?mbona hawatoi takwimu za madreva waliosababisha vifo vya abiria kwa uzembe,kwani huo sio ukiukwaji wa haki za binadamu,tatizo la awa watafiti wanafanya utafiti wakiwa biased.

    ReplyDelete
  3. Nadhani hata ninyi mpo biased na hanjui kama utafiti unalenga kundi au kitu fulani na sio kila kitu kama mnavyotaka iwe. Utafiti huu umesema ulicholenga, wengine wanaweza fanya utafiti wakalenga vifo vya kusababishwa na madereva au vifo vya askali vilivyosababishwa na raia. Watanzania tukomae kuhukumu watu visivyo.

    ReplyDelete
  4. Mapolisi wengi hawajaenda shule. kwanza upolisi wa sasa si wa wito ila ni wa kuganga njaa tu ndio maana hata rushwa wameizidisha. Mtu akiwasema kuwa wanakosa haki za kibinadamu anawaonea , hawaelewi kitu pale. Wapelekeni shule hao

    ReplyDelete
  5. Nidhamu katika jeshi la polisi ni mbaya sana, wamezidi kula rushwa. Wao wanachojua ni kupiga tu watu bila sababu. Manyanyaso yao kwa raia yamepita kipimo; wao ndio wamekuwa chimbuko la uvunjaji wa haki za binadamu hapa nchini, si hilo tu wamekuwa wanatumiwa vibaya na serikali hii dhalimu. Polisi wameshidwa kujitambua kuwa ni chombo huru na pia hakitakiwi kuwa na mwingilio wa chama tawala katika shughuli zake. Bila katiba mpya Haki za Binadamu ni ndoto !

    ReplyDelete