26 May 2011

Uongozi mbovu chanzo kufa Posta-Kamati

Na Edmund Mihale

KAMATI ya Kudumu ya Hesabu ya Mashirika ya Umma imesema kuwa uongozi mbovu wa Shirika la Posta ndio chanzo cha kufa kwa  shirika hilo.Hayo yaliwekwa
wazi Dar es Salaam jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Deo Filikunjombe ambapo alipingana na utetezi unaotolewa na uongozi wa shirika hilo kuwa limeshindwa kufanya biashara kutokana na kuingia kwa teknolojia mpya ya mtandao hatua iliyolifanya shirika hilo kufa.

"Sikubaliani na hili kuwa mtandao ndio sababu ya kufa kwa Shirika la Posta mbona huko ulaya yalikoanzia mambo hayo mashirika yake ni imara na yanafanya kazi vizuri hapa kwetu kwa nini ishindikane," alisema.

Alisema kuwa kushindwa kuthamini wafanyakazi kwa kuwalipa mishahara inayoridhisha ni chanzo cha kushuka kwa ufanisi katika shirika hilo.

"Mimi nimeozungumza na mmoja wa wateja wenu ambaye alinambia kuwa kuna siku alikuwa na barua 3,000 na alipowapigia simu kwa ajili ya kwenda kuzichukua iliwachukua siku tatu," alisema Bw. Filikunjombe.

Alisema kuwa uongozi huo umekuwa ukitumia fedha kwa fujo bila kuangalia pato lake na kutoa mfano kuwa linatumia zaidi ya sh. milioni 400 kwa ajili ya kuwafadhili watu wanaotaka kufanya nao biashara kwa kuwapa chai na soda bila kuangalia hali ya shirika.

Alieleza kuwa haoni umuhimu kuwa na wafanyakazi wengi ilihali wanashindwa kuwahudumia wateja wake.

"Mimi sioni umuhimu wa kuwa na wafanyakazi hawa 2,225 wakati unashindwa kulipa hata michango ya NPF na PPF, huyu mfanyakazi analipwa sh. 400,000 lakini anakatwa madeni hadi anabaki na sh. 1600 hivi atakuwa na akili ya kufanya kazi kwa bidii kweli wajalini wafanyakazi wenu," alisema.

Alisema kuwa shirika hilo linatakiwa kuweka mikakati itakayolipeleka mbele na kulitoa hapo lilipo.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliagiza shirika hilo kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na kamati.

Mapendekezo hayo ni kulipa pensheni ya wafanyakazi na mafao mengine, kulipa mishahara kwa wakati, kufuatilia madeni yanayodaiwa na shirika hilo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Bw. Deus Mdeme alikiri kuwepo kwa matatizo hayo kwa siku za nyuma lakini kwa sasa shirika hilo limejipanga kufanya vizuri na kuihakikishia kamati hiyo kuwa halitakufa huku akijigamba kuwa shirika hilo ni bora kuliko mashirika yote ya posta yaliyo Kusini mwa Janga la sahara.

1 comment:

  1. This is another mattaka,remove him out,we have very educated and exposed people in our contry why can't you use them

    ReplyDelete