Na Peter Ringi, Manyara
JESHI la Polisi mkoani Manyara linawashikilia watu 45 kwa tuhuma za kuvamia shamba la mwekezaji la Kiru Valley lililopo katika Bonde la Kiru wilayani Babati na kuteketeza
kwa moto matrekta mawili na kuiba mali za mwekezaji huyo.
Akithibitisha kutokea kwa uhalifu huo Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Bw. Parmena Sumary amesema jeshi hilo limeanzisha operesheni hiyo baada ya kuwabaini watuhumiwa wa matukio ya uvamizi wa mara kwa mara na kumsababishia mwekezaji huyo, Bw. Mukesh Organ hasara ya mamilioni ya fedha.
Kamanda Sumari alisema “Tukio la kuchoma matrekta na mashamba ya wawekezaji siyo mgogoro ya ardhi, bali huo ni uhalifu, hivyo wahalifu watasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mwishoni mwa mwezi uliopita watu wasiofahamika walivamia makazi hayo na kuwajeruhi baadhi ya wafanyakazi na kutia chumvi kwenye injini za matrekta na kuiba baathi ya vitu.
Bw. Sumary alisema jeshi lake limefanikiwa kuwanasa wakulima wadogo akiwemo mlemavu mmoja anayesadikiwa kuwa ni mganga wa kienyeji aitwaye Bw. Ramadhani Ginati (Ginyo) na wanawake wanane.
Bw. Sumary alizitaja sababu za kushikiliwa kwao ni uharibifu wa mali, wizi, uchochezi, kuingiza mifugo mashambani, na kuchoma mkaa vitendo ambavyo viko kinyume na sheria.
Kutokana na migogoro ya mara kwa mawaziri watano walitembelea eneo hilo Machi mwaka huu kuchunguza kiini cha vurugu hizo na kutoa agizo la kuundwa kwa kamati ya usuluhishi kati ya wakulima wadogo na wakubwa ambayo iliundwa mwishoni mwa Aprili.
Diwani wa Kata ya Kiru, Bw. Fabian Tlanka alisema yeye anaungana na Jeshi la Polisi kwa maamuzi yake ya kuwasaka na kuwatia mbaroni wote wanaojihusisha na uhalifu na uchochezi katika bonde hilo lenye mchanganyiko wa wakulima wadogo na wakubwa.
No comments:
Post a Comment