10 May 2011

Pensheni kupunguza mauaji ya vokongwe, ombaomba

Na Suleiman Abeid, Shinyanga
 
SERIKALI imeombwa kuwalipa pensheni wazee wote nchini kwa kuzingatia umri wao, hatua ambayo itasaidia kupunguza mauaji ya vikongwe nchini.Hayo yameelezwa
na Bw. Smart Daniel ambaye ni meneja miradi huduma za kijamii na afya kutoka Shirika la Helpage International na kufafanua kuwa utaratibu wa kuwalipa pensheni wazee kwa kuzingatia uzee wao utachangia ulinzi mkubwa kwa wazee hao.
 
Bw. Daniel alisema utaratibu mzuri wa kuwalipa pensheni wazee unaofaa ni ule ambao kiwango cha malipo yao kwa mwezi huongezeka kulingana na umri wa mtu, ambao inavyotumika nchini Mauritius.
 
“Hili suala la kuwalipa pensheni wazee wote linaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa ulinzi mkubwa wa wazee hao ndani ya familia, maana familia na ndugu watafahamu kadri umri wa mzee wao unavyoongezeka ndivyo mapato yake kutokana na pensheni yanavyoongezeka.
 
“Nchini Mauritius wazee wanalindwa sana kutokana na nchi hiyo kutoa malipo ya pensheni kwa wazee wote bila kujali iwapo awali walikuwa wafanyakazi, malipo ambayo huongezeka kadri umri wa mzee unavyoongezeka, familia zao huwalinda kwa kuwatunza ili waweze kujipatia kipato kikubwa,” alieleza Bw. Daniel.
 
Malipo ya pensheni kwa wazee wote bila kujali iwapo awali walikuwa wafanyakazi yatasaidia pia kupunguza tatizo la ombaomba katika miji mikuu kutokana na wazee wote kulazimika kuishi katika vijiji vyao ambako husajiliwa na kuratibiwa ili waweze kulipwa pensheni hiyo kila mwezi.
 
Alisema hapa nchini mfumo wa kuwalipa wazee wote wenye umri wa kuanzia miaka 60 pensheni ya kila mwezi haujaanza kutekelezwa japokuwa pamekuwepo
na mapendekezo mbalimbali yakishauri kuanzishwa kwa utaratibu huo.
 
“Mpaka hivi sasa ni asilimia nne pekee ya wazee ndiyo wanaopata pensheni, ikiwa ni wale waliokuwa wameajiriwa katika sekta rasmi ambao ni theluthi mbili ya wanaume wote nchini,” alieleza Bw. Danie.

No comments:

Post a Comment