Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MTUMISHI wa Shirika la Shirika la Umeme nchini (TANESCO) mkoani Shinyanga, Bw. Charles Ilomo amekamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani akituhumiwa
kwa kosa la kutishia kuua kwa kutumia bastola.
Bw. Ilomo ambaye pia anamiliki kampuni ya ukandarasi, anatuhumiwa kuwa Mei 10, mwaka huu alitishia kumuua kwa kumpiga risasi Katibu wa Sungusungu wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. John Kadama kwa madai ya kukataa kumpatia stakabadhi za malipo ya maombi ya zabuni kutoka Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu tukio hilo, Bw. Kadama alisema chanzo cha yeye kutishiwa kuuawa kwa kupigwa risasi ni kukataa kumpatia Bw. Ilomo baadhi ya stakabadhi ambazo alikuwa amelipia ada ya maombi ya zabuni ya kukusanya ushuru katika halmashauri hiyo.
Bw. Kadama alisema awali alikuwa amekubaliana na Bw. Ilomo amwazime leseni yake ya ukandarasi ili aombee kazi ya ukusanyaji ushuru katika minada iliyopo maeneo ya manispaa kwa makubaliano ya kumlipa kila mwezi kutokana na yeye kutumia leseni hiyo.
Alisema Bw. Ilomo alikubali kumwazima leseni hiyo na yeye (Kadama) aliomba kazi manispaa ambapo maombi yake yalikubaliwa na akapewa kazi ya kukusanya ushuru katika kata tisa za manispaa hiyo.
"Maombi yangu yalikubaliwa na nikatakiwa kulipa sh 1,370,000 ikiwa ni ada ya maombi ya zabuni, kinga na malipo ya mwanzo kwa ajili ya kazi hiyo na nikapewa stakabadhi zote kuthibitisha kwamba nimelipa malipo hayo," alieleza Bw. Kadama.
Hata hivyo, alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida baada ya yeye kukataa kumpatia Bw. Ilomo stakabadhi hizo ghafla alianza kumfokea kwa nguvu na kutishia kumuua ambapo alitoa mfukoni mwake hundi yenye thamani ya sh milioni 24 na kumweleza kama amegoma kutoa stakabadhi hizo, basi atahakikisha fedha hizo zinamtoa uhai.
"Kwa kweli nilishangaa na kushtushwa sana na hatua hiyo ya Bw. Ilomo, maana alisema iwapo kiasi kile cha fedha kisiponimaliza basi atatumia bastola yake kunitoa uhai, huku akinionesha bastola hiyo, wakati huo nilikuwa na Kamanda wa Sungusungu wa Kata ya Ndala, Bw. Thomas Mwita akishuhudia," alieleza Bw. Kadama.
Alisema baadaye Bw. Mwita alijaribu kusuluhisha tatizo hilo na Bw. Ilomo alikubali kurejesha silaha yake mfukoni na kisha yeye (Kadama) aliamua kwenda polisi kutoa taarifa ambao walimkamata Bw. Ilomo na kumfungulia shitaka la kutishia kuua kwa silaha.
Akizungumza na Majira kupitia simu yake ya kiganjani, Bw. Ilomo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari ameshapelekwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutishia kuua na kuwa hayo ni mambo ya kawaida tu.
Jeshi la polisi mkoani Shinyanga limethibitishia kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mtumishi huyo wa TANESCO na kesi yake ilitajwa juzi katika mahakama ya wilaya na imeahirishwa hadi wiki ijayo, mshtakiwa yuko nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment