01 June 2011

David Silva ampata tano Tevez kubaki Man City

LONDON, England

MSHAMBULIAJI wa Manchester City, David Silva amempa tano mshambulaji mwenzake Carlos Tevez, kwa kuamua kubaki katika klabu hiyo majira ya joto
yajayo.

Awali mchezaji huyo raia wa Argentina alikuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa kuondoka katika klabu hiyo ya Eastlands, licha ya kupata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na kufanikiwa kufuzu michuano ya Klabu Bingwa Ulaya hatua ya makundi msimu ujao.

Lakini Silva  hivi sasa anasema ana matumaini mchezaji huyo ataendelea kukipiga katika klabu hiyo msimu ujao.

“Nataka Tevez aendelee kubaki kwani ni mchezaji muhimu,” aliiambia The Manchester Evening News.

“Amefanya mambo mengi tofauti ndani ya timu hii,” aliongeza.

Wachezaji wote wawili, Silva na Tevez walikuwa nguzo muhimu katika kuisaidia Manchester City kutwaa ubingwa wake wa kwanza, ikiwa ni baada ya miaka 35 na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye michuano ya Ligi Kuu.

Hata hivyo, Mhispania huyo alikiri kwamba klabu hiyo itashindwa kupumzika na kuendelea katika mwenendo iliyonayo kwa hivi sasa na kukabiliana na changamoto, itakazokumbana nazo msimu ujao katika mbio za kuwania ubingwa, endapo haitambakiza Tevez ambaye ni kipenzi cha kocha wa timu hiyo, Roberto Mancini.

“Ni fahari kumaliza ligi tukiwa na ubingwa, nina imani tutaweza kushinda mataji mengine zaidi msimu ujao,” aliongeza mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment