01 June 2011

Copa Coca-Cola kutimua vumbi Juni 11

Na Addolph Bruno

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza ratiba ya mashindano Copa Coca-Cola ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ngazi ya taifa, ambayo
yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 11 hadi Julai 2 mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akitangaza makundi hayo mara baada ya droo iliyofanyika Dar es Salaam jana, Mratibu wa mashindano hayo kutoka TFF, Salumu Madadi alisema yamepangwa kwa makundi matano ambapo kila kundi linaongozwa na timu zilizotinga hatua ya nusu fainali msimu uliopita ambazo ni Kinondoni, Temeke, Kigoma, na Mjini Magharibi.

Alisema kundi A linaongozwa na mabingwa wa michuano hiyo msimu uliopita Kinondoni, Dodoma, Kusini Pemba, Singida, Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza ambapo kundi B lina timu za mikoa ya Temeke, Ilala, Kaskazini Unguja, Mtwara, Ruvuma, Manyara na Shinyanga.

Madadi alisema kundi C lina timu za Kigoma, Pwani, Kusini Unguja, Lindi, Rukwa, Tanga na Kagera huku kundi D limepangwa kuwa na timu za Mjini Magharibi, Morogoro, Kaskazini Pemba, Tabora, Iringa, Arusha na Mara.

Akizungumza kabla ya kufanyika kwa droo hiyo jana, Meneja Masoko wa Kampuni ya Coca-Cola, Alpha Joseph alisema timu hizo zitaanza kufanya maandalizi zikiwa kambini kuanzia Juni 6 mwaka huu Kibaha mkoani Pwani.

Alisema mwaka huu hamasa imeongezeka zaidi kama ilivyo kwa misimu mingine na kuomba wachezaji kuzingatia nidhamu katika ngazi ya taifa kuweza kufikia lengo na kuwaomba mashabiki wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kuwashangilia na kuwapa moyo vijana.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni aliyeambatana na Kocha Mkuu wa timu za vijana Mdenmark Jim Poulsen, alisema TFF inafurahi kuona wadhamini wakitimiza ahadi yao na kuwaahidi kuendeleza ushirikiano na kuwaomba vijana kuendelea kuonesha ushindani ndani na nje.

No comments:

Post a Comment