01 June 2011

Kaseja aumia taya, atemwa Stars

*Samatta, Ngassa wapasua vichwa makocha

Na Zahoro Mlanzi

KIPA wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Simba, Juma Kaseja ameumia taya wakati wa mazoezi na kwamba hatakuwepo katika
kikosi kitakachosafiri Juni 3, mwaka huu kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mbali na hilo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen atakuwa na wakati mgumu wa kuamua wachezaji Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta, Jabir Azizi na Kigi Makasi kuchezea timu yake au wakaisaidie timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23, inayokabiliwa na mchezo dhidi ya Nigeria.

Taifa Stars inatarajia kwenda nchini humo ikiwa ni mchezo wa kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba timu itaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Samwel Nyara kwenda nchini humo.

"Timu itakuwa na msafara wa watu 30, ambapo kati yao 20 ni wachezaji, wanne viongozi na sita ni kutoka benchi la ufundi ambapo kitaondoka Juni 3, mwaka huu badala ya Juni 4," alisema Wambura.

Alisema kipa Kaseja hatokuwepo katika msafara huo kutokana na kuumia taya, wakati wa mazoezi hivyo jana alitarajia kwenda kupiga X-ray ili kujua ukubwa wa tatizo hilo.

Wambura alisema kutokana na suala hilo, kipa Shaaban Kado ambaye pia ni kipa wa Vijana Stars moja kwa moja atakuwepo katika msafara huo pamoja na kipa Shaaban Dihile, hivyo hatokuwepo katika mchezo dhidi ya Nigeria.

Akizungumzia wachezaji wanaocheza soka la kulipwa (Maproo), alisema wote wameshafika isipokuwa Abdi Kassim 'Babi' na Danny Mrwanda ambao walitarajiwa kuwasili jana mchana na leo asubuhi Nizar Khalfan anatarajiwa kutua.

Wakati huo huo, Wambura alisema suala la wachezaji Ngassa, Samatta, Jabir na Kigi kuwepo katika timu mbili za taifa, alisema Poulsen ndiye atakayeamua wachezaji hao wachezee timu ipi.

Alisema leo wanatarajia kocha huyo awasilishe majina ya wachezaji watakaokwenda huko na kisha watachagua siku maalumu kwa ajili ya kutangaza rasmi wachezaji watakaoondoka.

No comments:

Post a Comment