Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakulima wanaolima kilimo cha umwagilia kupitia mto Ruvu ambako kuna chanzo cha maji cha mtambo wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (DAWASCO) wanahatarisha
maisha ya watumiaji wa maji hayo kutokana na matumizi ya dawa ya kuulia wadudu.
Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya mafunzo ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha kwanza wa shule ya Sekondari ya Bundikani ambao walifika eneo hilo kwa lengo la kuona namna maji yanavyoandaliwa hadi kuwafikia wanywaji.
Majira lilishuhudia wakulima hao wakiendelea na kilimo cha mazao mbalimbali jirani na chanzo hicho cha Ruvu Juu.
Licha ya serikali kuweka mipaka inayoonesha umbali unaopaswa kuachwa, wakulima hao wameingia jirani na chanzo hicho hatua inayohatarisha chanzo hicho.
Wakulima hao wamekuwa wakitumia dawa ambazo ni sumu kwa ajili ya kuua wadudu ambazo dawa hizo hutiririkia kwenye mto huo ambapo maji hayo huingia kwenye chanzo cha maji.
Mmoja wa wataalamu wa maabara ya kupimia maji kwenye mamlaka hiyo Bw. Jackson Mushi ambaye alisema kuwa yeye si msemaji wa mamlaka hiyo lakini alikiri kuwepo kwa tatizo hilo .
Bw. Mushi alisema wakulima hao wanakiuka taratibu zilizowekwa na serikali za kutolima jirani na eneo hilo lakini kutokana na kutochukuliwa hatua zozote wameendelea kulima na kutiririsha sumu kwenye chanzo hicho.
Naye Mwalimu Bw. Abdala Likava ambaye ni mkuu wa Idara ya Sayansi alisema kuwa lengo la ziara hiyo ya mafunzo ni kuhamasisha wanafunzi wa shule hiyo kupenda masomo ya Sayansi ambapo zaidi ya wanafunzi 30 walitemebelea chanzo hicho na kuangalia uzalishaji wa maji.
No comments:
Post a Comment