Na Zahoro Mlanzi
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), linatarajia kuijadili Yanga baada ya kuandika barua ya kuomba isamehewe au kupunguziwa
adhabu waliyopewa na baraza hilo.
Yanga ilifungiwa na CECAFA kwa utomvu wa nidhamu baada ya kushindwa kuingiza timu katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati dhidi ya Simba na kufungiwa miaka mitatu na kutozwa faini ya dola 35,000.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Yanga ukaliandikia barua baraza hilo huku ikidai itazilipa kwa awamu fedha hizo huku ikiomba kusamehewa au kupunguziwa adhabu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa baraza hilo, Leodgar Tenga alisema kweli wamepokea barua ya Yanga na kwamba Kamati yake ya Utendaji itakutana kujadili suala hilo.
"Lile ni jambo la ovyo sana kufanywa na Yanga, kushindwa kuingiza timu wakati mashabiki tayari wamelipa fedha zao na wapo uwanjani, lakini kama wameona wamefanya kosa na wameomba kusamehewa ngoja tuone itakuwaje," alisema Tenga.
Alisema kuomba msamaha ni jambo jema hivyo Katibu wake Mkuu, Nicholaus Musonye atawatafuta wajumbe wa kamati popote walipo watakutana na kisha watalitolea taarifa.
Wakati huo huo, Tenga alisema kutokana na hali ya machafuko yanayoendelea nchini Sudan, Kamati ya Utendaji ya CECAFA itakaa na kujadili kuona kama itawezekana mashindano hayo yafanyike Dar es Salaam.
Alisema mashindano hayo yanatumia gharama kubwa, hivyo anawaomba wadau mbalimbali wa soka wenye uwezo wa kugharamia mashindano hayo wawasiliane nao, ili yafanyike Dar es Salaam.
"Sudan hali si nzuri, kuna machafuko ya kisiasa, hivyo tunahitaji wadhamini na ikiwezekana yafanyike Dar es Salaam, sisi (CECAFA) tutagharamia usafiri wa ndani, posho za waamuzi na hoteli lakini mambo mengine tusaidiwe," alisema Tenga.
No comments:
Post a Comment