19 April 2011

Wezi wa mifugo wanyonga mtoto

Jamillah Daffo na Mary Margwe, Babati

WATU watatu wasiojulikana wakiwa na visu na mapanga wamemuua mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi ya Lotapesi na baadaye kuiba
ng'ombe 700 na mbuzi 200 katika Kitongoji cha wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Bw. Parmena Sumary, tukio hilo lilitokea aprili 16, mwaka huu majira ya saa 7.00 mchana huko katika Kitongoji cha Mbayeki wilayani humo.

Alisema kuwa siku tukio mtoto huyo, Noeli Simoni (13) akiwa na mdogo wake Naishoo, aliuawa kwa kunyongwa kwa kutumia shuka alilokuwa amevaa na watu wasiojulikana na baadaye kutoroka na mifugo hiyo.

Watoto hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakiwa wanachunga
kwenye mbuga hiyo ambapo watu watatu ambao hawakufahamika wakiwa na visu waliwakamata watoto hao na kumfunga mmoja shingoni kwa kutumia shuka lake na kuanza kumvuta hadi walipohakikisha amefariki dunia na kumuacha akiwa na majeraha kisha watu hao kuondoka na mifugo hiyo.

Amesema kuwa mdogo wa marehemu Naishioo alifanikiwa kutoroka na kwenda kutoa taarifa kwa nyumbani kwao, ingawa hakuwakuta wazazi wao lakini wananchi walijitokeza na kwenda kufuatilia tukio hilo na kumkuta mwenzake alikwishauawa.

Kamanda Summary alisema kuwa baada ya wananchi kufuatilia mifugo hiyo walifanikiwa kuokoa ng’ombe 700 na mbuzi 130 ambao walikuta  wametelekezwa katika maeneo ya kitongoji hicho. Mbuzi 70 hazijapatikana.

Naishoo alikimbizwa katika zahanati ya kijiji cha Sunya kwa matibabu na hakuna mtu aliyekamatwa na juhudi za kuwatafuta wahusika zinaendelea.

1 comment:

  1. Mungu amlaze maali pema peponi mtoto huyo aliyeuwawa kikatili na watu wasio na huruma. Auwae kwa upanga nae pia auwawe kwa upanga, hao watu waliomyonga huyo mtoto ambaye ana hatia nao wauwawe kwa kunyongwa kupitia adabu Mwenyezi MUNGU anayowapa.

    ROHO YA MAREHEMU ILAZWE MAHALI PEMA PEPONI>
    AMINA

    ReplyDelete