08 April 2011

Viongozi CCM Mbarali waonywa

Na Esther Macha, Mbarali

SAKATA la Mbunge wa Mbarali (CCM), Bw. Dickison Kilufi kufanyiwa njama za kutaka kunyang’anywa kadi ya uanachama limeingia katika sura mpya baada ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kuwaonya viongozi wa ngazi ya wilaya wasithubutu kufanya hivyo kwa sababu hawana uwezo wala mamlaka ya kufanya hivyo.

Akizunguma na gazeti hili jana, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Bi. Verena Shumbusho alisema viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya hawana madaraka kumnyang’anya kadi mbunge, hivyo kama kweli wanafanya njama hizo wanajidanganya.

Mbunge wa jimbo hilo anafanyiwa njama hizo hizo kutokana na kuwa na msimamo tofauti na viongozi wa chama na serikali ya wilaya na mkoa kuhusu mgogoro unaoendelea kufukuta kati ya wananchi wa wilaya ya Mbarali wanaomlalamikia mwekezaji wa shamba la mpunga la Mbarali Estate kuwanyanyasa.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wananchi walisema hatua hiyo ni ya hatari kwa kuwa  waliomuweka mbunge huyo madarakani ni wananchi kwa kumchangia fedha ya kuchukulia fomu ili kuwa mwakilishi wao.

Walisema msimamo wa mbunge kufuatilia haki na maslahi ya wananchi wa wilaya hiyo kunamfanya aonekane yupo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na hali hiyo inatokana na mwekezaji wa shamba la mpunga la Mbarali Estate kuwa na mgogolo na wananchi wa Wilaya hiyo.

“Sisi ndiyo tuliompa ridhaa Bw. Kilufi kuwa mbunge, na maamuzi hayo yanayoshinikizwa na kundi la watu kwa maslahi yao binafsi yataigharimu serikali, kwani na sisi hatutakubali sauti yetu ikazimwa, tumempeleka bungeni akawe mwakilishi wetu,” alisema Lusekelo Mwilongo.

Bi. Lucy Msemwa alisema mbunge huyo ni maskini na hali ndiyo inayomfanya awatetee wanyonge, huku wananchi wakiamini kuwa ni msaada wao mkubwa, na hali hiyo baadhi ya watu wanataka kumtumia kwa maslahi yao jambo ambalo mbunge amekuwa akilipinga na wao kumuona hawafai na kufikia hatua ambayo itajenga historia.

No comments:

Post a Comment