Na Athman Hamza
MANISPAA ya Kinondoni imelazimika kutoa ufafanuzi wa sakata la kulipa mishahara hewa lililoibuliwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Bw. Ludovic Utouh.
Katika taarifa ya CAG iliyotolewa Jumanne wiki hii mjini Dodoma na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari ilionesha Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na Manispaa ya Kinondoni kuwa vinara wa ulipaji wa mishahara hewa kwa kupitia akaunti za benki kwa wafanyakazi waliofariki dunia, wastaafu, watoro, waliooacha kazi na waliofukuzwa.
Akizungumza na Majira jana Ofisa Mahusiano wa Manispaa hiyo, Bw. Sebastian Mhowera amesema mpaka sasa manispaa yake haijapata taarifa kamili ya kimaandishi kuhusu suala hilo na kusema amelazimika kuelezea hali hiyo ili kutoa ufafanuzi kwa jamii kuhusu uhalisia wa suala hilo.
Bw. Mhowera alisema sio mara ya kwanza kwa manispaa yake kupata taarifa kama hiyo kwani katika taarifa kama hiyo ya mwaka 2008/2009 Manispaa hiyo ilionekana kulipa mishahara hewa lakini baada ya kufanyika uchunguzi ikagundulika fedha hizo hazijalipwa kama ilivyodaiwa.
Akielezea tatizo liliopo na sababu ya kurudiwa kwa taarifa hizo, alisema inatokana na wakaguzi wa nje kuamini misharaha inaendelea kuja kutoka hazina wakati watumishi hawapo jambo ambalo anasema sio tatizo lao kwani hazina bado hawajafuta majina ya wafanyakazi hao.
Alisema, baada ya mfanyakazi kuacha kazi, kufariki au kufukuzwa Manispaa hukatisha malipo yote “stop payment order” ndani ya mwezi mmoja na kutuma fedha hizo kwa Ofisa Tawala wa mkoa (RAC) kama inavyotakiwa kufanywa.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2009/2010 Manispaa ya Kinondoni ilirudisha jumla ya sh. milioni 85.9 kiasi ambacho ni zaidi ya kile kilichotajwa katika taarifa ya CAG .
No comments:
Post a Comment