Na Suleiman Abeid, Maswa
WATU watatu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi wamekufa huku mmoja akinusurika kifo kwa kukimbilia katika Kituo cha Polisi baada ya kushambuliwa kwa
kipigo na wanakijiji wenye hasira wakiwatuhumiwa kwa kosa la kuvunja maduka matatu na kuiba.
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Malampaka, Bw. Peter Mahuiga tukio hilo lilitokea saa 11 alfajiri juzi wilayani Maswa mkoani Shinyanga.
Kati ya watuhumiwa hao mmoja aliyetambulika kama Bw. Thomas Ngussa (40) mkazi wa Kitongoji cha Mwenge Malampaka na mwingine kwa jina moja la Bw. Mashaka jina ambalo lilikutwa katika tiketi ya kusafiria ikionesha alitoka Mwanza kwenda Shinyanga.
Bw. Mahuiga alisema chanzo cha mauaji hayo kilitokana na watuhumiwa hao kuvamia katika kijiji hicho juzi alfajiri na kuvunja maduka matatu ya wafanyabiashara na kupora mali mbalimbali ikiwemo fedha taslimu.
Alisema wananchi hao nusura wakishambulie pia Kituo cha Polisi wakimfuata mmoja wa watuhumiwa aliyekimbilia katika kituo hicho ambako alijisalimisha na kuokolewa na polisi waliofyatua risasi hewani kuwatawanya wanakijiji hao.
Akifafanua, alisema baada ya kupatikana kwa taarifa za kuvunjwa kwa maduka hayo wamiliki wake walipiga yowe la kuomba msaada kutoka kwa wanakijiji ambao walifika na kuanza kuwasaka watu waliohusika na wizi huo kwa kushirikiana na sungusungu.
Wanakijiji hao walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kabla hawajatokomea mbali wakiwa na baadhi ya mali zilizokuwa zimeibwa katika maduka hayo ambapo walianza kuwahoji na wao kukiri kutenda kosa hilo.
Baada ya kuwahoji na kukiri kuhusika na uvunjaji wa maduka hayo, wanakijiji ndipo walipochukua uamuzi wa kuwashambulia kwa kipigo cha fimbo na mawe wote watatu hadi wakafa, na baada ya kuhakikisha wamekufa wanakijiji wote walitawanyika na kurejea makwao, alieleza Bw. Mahuiga.
Alisema taarifa zilifikishwa katika Kituo cha Polisi wilayani Maswa na walifika na kuwachukua viongozi wa
serikali ya Kitongoji, Kijiji pamoja na Kata kwa ajili ya mahojiano wilayani Maswa.
Baada ya wanakijiji kupata taarifa za kukamatwa kwa viongozi wao waliamua kuandamana kwa kutumia magari matano aina ya Fuso kwenda wilayani ili kutaka kufahamu sababu za kukamatwa kwa viongozi wao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa tuko hilo japokuwa alikanusha madai ya wananchi kuandamana kwa lengo la kushinikiza kuachiwa huru kwa viongozi waliokuwa wanahojiwa na polisi.
Hata hivyo habari kutoka wilayani Maswa ambazo pia zimethibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kapteni James Yamungu, zimeeleza kuwepo kwa maandamano hayo ya malori matano yaliyokuwa yamewabeba wanakijiji hao kutoka Malampaka kwenda mjini Maswa, ambapo hata hivyo safari yao iliishia njiani baada ya kukutana na viongozi wao wakirudi
nyumbani.
"Ni kweli nilipata taarifa za kuwepo kwa magari matano yaliyokuwa yamewabeba wanakijiji cha Malampaka wakija mjini kutaka kushinikiza kuachiwa kwa viongozi wao waliokuwa wakihojiwa na polisi, lakini nimepata taarifa walikatisha safari yao baada ya kukutana na viongozi wao wakirejea nyumbani," alieleza mkuu wa wilaya, Kapteni
Yamungu.
No comments:
Post a Comment