31 March 2011

Mroso atamba 'kumtemea sumu' Maneno Osward

Na Addolph Bruno

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Robert Mroso 'Cobra' wa Arusha ametamba kumchapa mpinzani wake, Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' katika pambano
litakalochezwa Jumamosi katika Ukumbi wa Amana Jijini Dar es Salaam.

Pambano hilo lisilo la ubingwa, litakuwa ni la raundi 10 uzito wa kati (middle) ambalo limeandaliwa na Rajab Mbogo.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mroso alisema anatarajia kuchukua ushindi dhidi ya Mtambo wa Gongo kutokana na kufanya maandalizi ya kutosha, akiwa kambini jijini Arusha kwa ajili ya kuweka rekodi yake sawa.

"Nimefanya maandalizi ya kutosha mno na anatarajia nitakuwa mshindi ingawa chochote kinaweza kutokea, nataka kuiweka vizuri rekodi yangu na ninamfahamu vizuri Maneno asitarajie kushinda kwangu," alisema Mrosso.

Kwa Upande wake Mratibu wa pambano hilo, Mbogo alisema lengo la pambano hilo ni kuendeleza viwango vya mabondia hao kwa kuwapatia mapambano ya mara kwa mara na kwamba maandalizi yote yamekamilika.

Alisema mabondia hao watapimwa uzito na afya zao siku moja kabla ya pambano hilo kupigwa ambalo linatarajia kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na mabondia hao kukamiana tangu muda mrefu.

Mbogo alisema mchezo huo utatanguliwa na mambano mengine ya raundi nne ya uzito tofauti ambapo bondia saleh Mkalekwa atacheza na Aogwa Mwita, Hamisi Juma dhidi ya Maulid Bakari, wakati Maneno Jokoro atapambana na Omari Bomba.

No comments:

Post a Comment