Na Mwandishi Maalumu
SIKU tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kurudi nchini akitokea ziarani Ufaransa na Ivory Coast, jana aliondoka tena kwenda kuungana na marais wenzake
wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Rais Kikwete na wenzake wanakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, katika jitihada mpya za kutafuta jawabu la mzozo huo uliolipuka mwishoni mwa mwaka jana kufuatia matokeo ya raundi ya pili ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 28, 2011.
Katika mkutano huo wa siku mbili, marais hao wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao kwa Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika (AU), ili kuuwezesha umoja huo kuchukua uamuzi kamili wa jinsi ya kumaliza mgogoro huo.
Ripoti hiyo ni matokeo ya mikutano ya marais hao mjini Addis Ababa, Mauritania ambako walikutana mara mbili, na mjini Abidjan, Ivory Coast. Marais hao waliteuliwa na Kikao cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU katika mkutano wao wa Januari mwaka huu.
Rais Kikwete aliondoka jana asubuhi kwenda Ethiopia kwa kikao hicho cha siku mbili ambako ataungana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Idriss Deby wa Chad, Rais Blaise Campaore wa Burkina Faso na Rais Mohamed Abdel Aziz ambaye ni mwenyekiti wa kundi hilo.
Wengine wanaotarajiwa kushiriki katika kikao hicho ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Bw. Jean Ping na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa (UN).
Mzozo wa Ivory Coast ulianza baada ya taasisi mbili zinazosimamia uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo tofauti ya washindi wa raundi hiyo ya pili ya upigaji kura kati ya Bw. Laurent Gbagbo, aliyekuwa anatetea kiti chake na mpinzani wake mkuu, Bw. Alassane Quattara.
Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Bw. Quattara kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia tisa, lakini siku nne baadaye, Baraza la Katiba la nchi hiyo lilimtangaza Bw. Gbagbo kuwa mshindi kwa asilimia moja.
Baraza hilo lilimtangaza Bw. Gbagbo mshindi baada ya kuwa limefuta matokeo katika majimbo saba aliyokuwa ameshinda Bw. Quattara, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko ngome kuu yake ya kisiasa. Kwa kufuta matokeo katika majimbo hayo, Baraza lilimpunguzia Bw. Quattara kura 600,000.
Tangu wakati huo, viongozi hao wawili walijitangaza marais na kila mmoja kuunda serikali yake. Nchi hiyo sasa imetumbukia katika mgogoro kamili wa kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambako yamekuwepo mauaji ya watu na uharibifu mkubwa wa mali.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Bw. Shabani Gurumo kuwa Mnikulu wa Ikulu.
Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemon Luhanjo jana ilisema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja.
Kabla ya uteuzi wake, Bw. Gurumo alikuwa Naibu Katibu wa Rais. Bw. Gurumo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Marehemu Rajab Kianda ambaye alifariki dunia Februari 7, mwaka jana, 2010.
Mnikulu ndiye msimamizi mkuu na kiongozi wa shughuli zote za nyumbani za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia yake, na pia ndiye mkuu wa watumishi wote wanaohusika na shuguli hizo.
Aidha, Mnikulu ndiye msimamizi wa Ikulu na Ikulu Ndogo zote nchini na ndiye hukaribisha mabalozi wapya wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania wanapokwenda Ikulu kukabidhi Hati za Utambilisho wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Endelea kutumia muda mwingi kutatua mambo ya watu wakati kwako kuna matatizo mengi lukuki. Huu ni utoto wa kufikiri. Huyu jamani siyo rais wetu labda wa ivori.
ReplyDeleteana nguvu za kuzunguka sasa si alienda kwa babu loliondo kupata ile kitu ya kutibu nanii..... yuko fit akirudi ethiopia labda atakua na afueni ya kutatua matatizo ya wananchi
ReplyDelete