02 March 2011

Hotuba ya Kikwete moto

*Yadaiwa haijaeleza suluhisho la matatizo
*CCM waifagilia, wasema ilikuwa ya faraja


Na Tumaini Makene

HOTUBA ya mwisho wa mwezi Februari ya Rais Jakaya Kikwete, imepokewa kwa
hisia tofauti, huku ikielezwa na wengi kuwa imeshindwa kuonesha mtazamo mpana juu ya chanzo na suluhisho la matatizo yanayoikabili nchi na jamii ya Watanzania kwa sasa.

Wakazi wasomi na baadhi ya wananchi wameikosoa wakisema kuwa tishio kubwa la usalama na mstakabali wa nchi kwa sasa si vyama vya siasa, bali ni kushindwa kwa mfumo wa uzalishaji mali na siasa, makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameipongeza wakisema ilikuwa ya faraja ambayo imeeleza matatizo makubwa ya nchi.

Hayo yamekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kutoa hotuba yake ya kila mwezi kwa taifa, ambapo kati ya masuala aliyoyazungumzia ni pamoja na suala la hali ngumu ya maisha inayoongeza umaskini miongoni mwa wananchi, huku bei za bidhaa muhimu zikizidi kupaa.

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alikiri kuwepo kwa ugumu wa maisha ya Mtanzania unaosababisha matatizo kadhaa, lakini akawaomba kuyakabili kwani yote hayawezi kuisha haraka kama ambavyo Watanzania wengi wanapenda iwe.

Rais Kikwete alisema kuwa serikali imeelekeza nguvu na raslimali zake katika nyanja mbalimbali hivyo kikwazo si upungufu wa sera wala dhamira, bali kikwazo kikubwa ni kiwango kidogo cha maendeleo ya kiuchumi nchini, huku pia akilinganisha hali ilivyo bora sasa kuliko katika awamu tatu za serikali zilizopita, kuanzia wakati wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Ubovu wa mfumo wa uchumi


Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Dar es Salaam (CKD), Bw. Bashiru Ally, alisema kuwa ni wakati mwafaka kwa nchi kukaa chini kufikiria kwa mapana chanzo hali cha matatizo yanayoikumba nchi kwa sasa, badala ya kushughulika na dalili zake, ikidhaniwa kuwa ndiyo vyanzo.

"Nafikiri kuna tatizo katika namna tunavyoyaona na kuyaeleza matatizo yetu na vyanzo vyake, ni kweli rais kazungumza vitu vya msingi kabisa, lakini tatizo ni namna anavyoonekana kuhitimisha, ni kama kwamba hatuna tatizo kabisa katika sera na mfumo wetu wa uzalishaji mali, bali inaonekana kwamba tatizo liko katika uwezo wetu, hilo ndilo tatizo tulilonalo.

"Kuna tatizo kubwa katika sera na mfumo wetu wa uzalishaji mali tuliokumbatia, na haya yanayoonekana ni dalili tu za ubovu wa mfumo wetu huo unaopelekea sekta muhimu kama ya kilimo kutoa mchango mdogo sana katika pato la taifa.

"Mfumo unaotufanya tunaua wakulima wadogo kwa kuwanyang'anya ardhi...tunapaswa kufikiria kwa mapana, chanzo cha mtatizo yanayosababisha mfumo wa siasa kufeli, mfumo wa demokrasia kufeli, kiasi ambacho watu hawataki kupiga kura, mfumo wa elimu umefeli kiasi ambacho nusu ya watahiniwa wamefeli mitihani," alisema Bw. Ally.

Alisema ni vyema Tanzania kama nchi ikatafakari kwa kina mfumo huo iwapo unaweza kusaidia kilimo kinachokufa, ukosefu wa ajira kwa waliosoma na wasiosoma, watu kukatishwa tamaa na michakato ya kidemokrasia kama vile kupiga kura.

"Sasa hivi ni baadhi ya vitu unapovichambua unaonekana wewe ni mtu wa ajabu, ndiyo maana hata rais analalamika juu ya CHADEMA. Ukiangalia kwa undani haya si matatizo ya CHADEMA...CHADEMA hawakuwepo kule Darajani (Zanzibar) ambako vijana wamachinga waliandama na kupambana na askari.

"Matatizo ya Darajani hayana tofauti na matatizo ya maeneo mengine, CHADEMA hawako katika uporaji mkubwa wa ardhi ya wakulima wadogo ambao sasa tunawaona wanajitokeza kupambana na wawekezaji wakubwa.

"Hawako katika uporaji mkubwa unaofanyika katika raslimali zetu kama vile madini, hawako katika kufeli kwa nusu ya wanafunzi wetu...bali ni mfumo unaotugawa vibaya kiasi ambacho pengo la walionacho na wasionacho ni kubwa sana," alisema Bw. Ally na kuongeza;

"Ni wakati mwafaka tukakaa chini na nafikiri moja ya nafasi ni katika mjadala wa katiba mpya, tutafakari mfumo wa uzalishaji mali, tutafakari mfumo wetu wa siasa, tujadiliane kwa kina...tujadili juu ya miiko ya uongozi, si maadili, miiko ya uongozi, tuweke wazi ukitaka kuwa tajiri uende kwenye sekta binafsi.

"Huwezi kuwa na serikali iliyojaa wajasiriamali, walanguzi, kisha ukatarajia watatoa huduma kwa wananchi, huwezi kuzungumzia hali ngumu ya maisha lakini serikali haiendani na hali hiyo...wananchi wana maisha magumu lakini juzi wanasikia wabunge wanakopeshwa milioni 90, hapo watu watakuwa na hasira tu, hawawezi kuvumilia viongozi walanguzi.

Hotuba ya faraja

Kwa upande wake, mmoja wa wanasiasa waandamizi nchini, Bw. John Chiligati alisema kuwa hotuba ya rais ilikuwa ni 'faraja' kwa sehemu kubwa, kuanzia kwa waathirika wa mabomu, waliokumbwa na uhaba wa chakula na wapenda amani ya nchi, kwani Rais Kikwete alikemea uchochezi unaofanywa na wanasiasa hata kuhatarisha amani ya nchi.

"Hotuba ya rais kwa kiasi kikubwa imetuliza wasiwasi uliokuwepo...ilikuwa ni ya faraja...wenzetu waliopatwa na athari ya mabomu huko Gongolamboto imewapatia faraja kubwa sana kwa kujengewa nyumba zao...suala la ukame ambalo limeleta tishio la chakula pia kalizungumzia akisema kuwa kuna tani zaidi ya elfu moja, hayo ni matumaini makubwa.

"Lakini pia kwa sisi wapenda amani ya nchi imetupatia faraja baada ya kukemea matamshi yanayoashiria vurugu nchini...hivi kweli mwanasiasa anakwenda kusema kuwa tutafanya kama Libya, anajua maana ya siasa kweli huyo, maana vurugu hazina macho, waangalie kwa mapana, kwa kweli imetupatia faraja sana hotuba hiyo," alisema Bw. Chiligati.

Kwa upande wingine Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Tambwe Hiza alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete ilikuwa nzuri, ikiweka mambo mengi wazi kwa mtu yeyote kuweza kuelewa uhalisia wa mambo yanayoendelea nchini.

Alisema kuwa Rais Kikwete ama ilivyo kawaida yake, alitumia hali ya utulivu na ukweli kufikisha ujumbe mahsusi kwa wananchi wake.

"Kwa kifupi hotuba ilikuwa nzuri sana, kwa kweli kwa mtu yeyote ambaye hana jambo lolote, ila anataka kujua hali halisi, rais ameeleza kila jambo vizuri sana, kwangu mimi nimeshika mambo manne kwa haraka...kwanza suala la Dowans ambalo watu wanapenda kulisema lakini wanalipotosha kwa kutumia uongo.

"Ameliweka sawa kama alivyosema Dodoma kuwa maamuzi ya kamati kuu na yale ya kamati ya wabunge wa CCM ni kuwa suala la Dowans lisubiri mahakama, lakini watu wanapotosha ikilipwa itakuwa hivi, kwani wanasema hivyo mwenye mamlaka ameshakubali kulipa," alisema Bw. Hiza.

Naye Katibu wa CCM wilaya Kilindi mkoani Tanga Bw. Aluu Segamba amesifu hotuba ya Rais Kikwete na kusema imeibua matumaini mapya kwa Watanzania hususani kwa hatua ya serikali yake kuchukua jukumu la kuwajengea nyumba waathirika.

"Rais amefanya jambo jema sana kuamua kuwajengea nyumba wananchi hao, bila kufanya hivyo wangeingia waliomo na wasiokuwe kwa lengo la kutaka kujinufaisha," alisema Bw. Segamba.

Akizungumzia kauli ya Rais Kikwete kuhusu CHADEMA alisema ametumia lugha ya upendo na uugwana kushauri chama hicho kuepusha vurugu kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa Watanzania.

Alisema maendeleo si jambo linalofikiwa kwa miaka 40 au 50 bali ni mchakato wa mrefu hata Marekani iliendelea baada ya miaka mingi huku ikiungana majimbo 51.

Kukabili majanga


Kwa upande wake Dkt. Peter Bujari alisema kuwa nchi inahitaji suluhisho la muda mrefu ili kukabiliana na madhira yanayowakabili wananchi na nchi kwa ujumla, badala ya kutegemea mipango ya muda mfupi.

Alisema kuwa viongozi watapoteza heshima mbele ya jamii iwapo hawatakuwa makini katika sera za kupunguza umaskini hasa kwa kujikita katika kunusuru upatikanaji wa nishati ya uhakika katika nyanja za umeme na mafuta ambazo ndizo zinagusa maisha ya kila siku ya kila Mtanzania.

"Nilimsikiliza rais kidogo, mchango wangu unaweza kuwa katika maeneo kadhaa...katika suala la mabomu ya Gongolamboto, ingawa serikali imeonesha kitu kizuri kwa kuamua kuwajengea nyumba walioathirika, yaani ime-sympathise nao (imewahurumia), lakini rais alipaswa kutuambia namna gani majanga kama hayo hayatajitokeza tena.

"Yaani badala ya kuzungumzia crisis management (utatuzi wa migogoro), tulipaswa kuzungumzia preventive management (uzuiaji wa majanga ya aina hiyo), angetupatia uhakika wa kutotokea kitu kama hicho, maana kilitokea mwaka 2009, kisha 2011, hilo la mikakati ya kuzuia milipuko isitokee tena hakuligusia.

"Katika suala la umeme rais alizungumza kina cha maji katika mabwawa yetu kilivyoshuka na mipango mingine ya serikali ya kupata umeme kama huko Mwanza na kadhalika...lakini suala kubwa kwangu ni mstakabali wetu kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa yaliyopo sasa na yanayotarajiwa miaka ishirini ijayo.

"Katika hali kama hiyo ni hatari sana kwa nchi kutegemea umeme wa maji. Tunavyo vyanzo kadhaa vinavyoweza kuchochea umeme mwingi tu, mathalani upepo wa Singida una unavuma kwa kasi na una uwezo wa kuzalisha umeme mara tatu zaidi ya ule upepo wa nchi za Scandinavian (Norway, Sweden, Denmark, Finiland).

"Lazima tupunguze utegemezi wa mvua, kuna vyanzo vya umeme pale Rufiji ambavyo zikifungwa mashine tatu tuna uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 kila mashine ikizalisha megawati 700, na sisi mahitaji yetu ni megawati 900, kunatakiwa long term solutions (mipango ya muda mrefu ya ufumbuzi).

"Lazima tukubali kuingia gharama katika kuwekeza ili tutumie gharama kidogo wakati wa uendeshaji badala ya sasa ambapo tunategemea maji na mafuta ambayo ni ghali sana, pia kukitokea rabsha tu katika nchi kama Libya zinazozalisha mafuta, hata sisi pia tunaathirika,' alisema Dkt. Bujari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Human Develompent Trust (HDT).

Katika suala la uzalishaji wa chakula cha kutosha alisema ni vyema mkakati wa kilimo kwanza ukajikita katika kilimo cha umwagiliaji badala ya kununua matrekta kwa kila kijiji au kata, kwani si maeneo yote yanahitaji zana hizo za kilimo, hivyo kusababisha upotevu wa fedha.

Akizungumzia kupanda kwa gharama za maisha, Dkt. Bujari alisema kuwa ni matokeo ya mzingo/mzunguko wa umaskini, unaosababishwa na ukosefu na kupanda kwa bei ya vitu muhimu kwa uchumi kama nishati ya umeme na mafuta, ambavyo athari yake ni kubwa katika sekta karibu zote za uzalishaji.

Suala jingine alisema ni kushuka kwa thamani/nguvu ya sh. ya Tanzania dhidi ya fedha nyingine katika soko la dunia, ambapo kwa miaka 15-20 iliyopita, fedha hiyo imepungua kwa kasi kutokana na nchi kushindwa kuuza bidhaa katika soko la dunia, kwani hakuna uzalishaji wenye tija na fanisi hasa katika eneo la viwanda.

"Iwapo mikakati ya kulenga watu wengi itazidi kuwa butu, watu watazidi kuwa maskini kuliko hivi sasa, umaskini utaongezeka sana na watu watakata tamaa na uongozi utakosa heshima," alisema Dkt. Bujari.

Sukari si tatizo pekee


Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Malamilo John, mkazi wa Kigamboni alisema kuwa itakuwa vigumu maendeleo kupatika iwapo ufisadi hautapigwa vita kwa nia na dhamira thabiti, kwani unaathiri nyanja zote za uchumi nchini.

Alisema iwapo Serikali ya Rais Kikwete, ingeamua kuwa makini na kushughulikia matatizo na kero za wananchi, wapinzani wangekosa cha kusema hata kupunguza uungwaji mkono wanaoupata sasa.

"Unajua bwana, bei ya vitu haijapanda katika sukari tu, imepanda karibu kila mahali, lakini pia uongozi tulionao hata ukitoa maelekezo hayafuatwi, labda kwa sababu wao hawanunui katika maduka tunayonunua sisi, lakini hakuna mahali sukari inauzwa sh. 1,700, karibu kila sehemu ni sh. 2,000 mpaka 2,200, sh. 1,700 ni bei ya kufikirika tu.

"Lakini pia katika suala jingine, rais atambue kuwa CHADEMA hawakumwambia kuwa alete maendeleo ndani ya siku tisa, walichosema wao ni kuwa ndani ya siku hizo atoe kauli juu ya hoja zao, wananchi wanawaunga mkono CHADEMA kwa sababu wanazungumzia kero hizo, kama serikali wakiyafanyia kazi moja baada ya jingine, watakosa agenda.

"Lakini pia rais hataki kulisikia hili suala la ufisadi, ufisadi unaathiri nyanja zote za uchumi, ikiwemo hata hiyo kilimo kwanza...kwa mfano walioweka ten percent kwenye ndege ya rais hawawezi kushindwa kufanya hivyo kwenye ununuzi wa matrekta, barabara badala ya kujenga kwa shilingi moja, tunatumia shilingi tatu.

"Fedha ambazo zingetumika kusaidia mahali pengine, zinaliwa na watu wachache wasiochukuliwa hatua," alisema Bw. John.

8 comments:

  1. tupewe mikakati ya kutuondolea umaskini siyo kukwepa kwa kuwatupia wengine mpira,serikali haitokwepa lawama watu wameshakuwa waelewa sana ni vema kusoma alama za nyakati

    ReplyDelete
  2. Tukubaliane na bwana Bashiru Ally kuwa nchi yetu ina tatizo la mfumo na sera...Napingana na Rais anayedai tatizo sio sera na dhamira... Kama kungekuwa na sera na dhamira:
    1. Kusingekuwa na shule za watoto wa vigogo na za kata ambazo hazina walimu.
    2.Kusingekuwa na mijadala ya kifisadi maana kungekuwa na miiko inayoheshimiwa na wote bila kujali ukaribu wao na Rais
    3. Kusingekuwa na hukumu ya kifungo ama faini kwa Chenge na wiki mbili baadae mtu akahukumiwa kifungo bila faini kwa kosa kama lake.
    4. tatizo la umeme lingekuwa historia maana vipaumbele sahihi ndivyo vingeanza kushughulikiwa... Kama tulitoa zaidi ya trilioni moja kwa jina la dharura kwa wanunuzi wa pamba, tunashindwaje kuwekeza kwenye umeme.
    5.Tusingeusikia upuuzi tuliosikia eti rais wetu anatakiwa kuwa na ndege kama za marais wenzake wakati wafanyakazi wa Tanzania kuongezewa maslahi ili waishi kama wafanyakazi wa mataifa mengine haiwezekani.
    Ni ajabu kuwa na rais anayeishi kama marais wa dunia ya kwanza na tunajitahidi asikose wanavyopata lakini wananchi waishi kama watu wa dunia ya sita, maana hata hiyo ya tatu haipo
    6.Tusingekuwa na rais na waziri mkuu anayenung'unika badala ya kuchukua hatua.
    Nchi inataka mifumo thabiti itakayokuwa na miiko na sera imara ambazo hazitategemea nani au chama gani kipo madarakani

    ReplyDelete
  3. Jaman makada wa CCm kila siku yenu kusifia,
    tehtehe! sijacheka!
    Nchi na wana wa nchi wamfikia hali hii kutokana na sera za CCM.
    sasa Raisi toa Dira ya nchi, Vijana hatuna kazi
    wategemea tuendelee kusoma alafu tukose ajira?
    Ya nini? Mwisho wa siku tutawakurupusha ka Misri na Libya.
    CCM KESHENI MAANA MWANA WA MAANDAMANO ANAKUJA SIKU NA SAA MSIYO IJUA!
    jAMAAN nJAA NA MAISHA MAGUMU?

    ReplyDelete
  4. Muheshimiwa rais acha kuwapa madaraka jamaa zako ambao kutwa wao wanajua unawalinda na ndiyo maana hawawajibiki na kufata maadili ya kazi. Hivi kweli hizi kero za watu na matatizo tuliyonayo unaweka watu ofisini na suti zao wanafanya kazi kwa simu unategemea nini?miradi yote inakufa,maendeleo yetu yanarudi nyuma badala ya keanda mbele huko mikoani usiseme mwananchi wa kawaida nchini kwetu hana haki na hana pakukimbilia watu wamewachoka unampa mtu madaraka kutumikia umma yeye anataka kwanza awe tajiri maana alikuwa anadharauliwa huu muda wako uliobaki kuwa DICTATOR fukuza wazembe wote mafisadi weka jela au hata kunyonga vunja baraza la mahakimu uanze usajiri mpya,fukuza mapolisi wote fisadi naamini watakulinda na ndiyo itakuwa njia pekee ya kuikoa CCM 2015. Muheshimiwa waziri mkuu kuwa kama Marehem SOKOINE usiwachekee nchi yetu wasiifanye HOLLYWOOD Wanakuja wanachota wanaingia mitini mungu tusaidie.mdau

    ReplyDelete
  5. Unajua hawa makada hawaelewi hata maana ya SERA. Wakisikia sera wanajua SARE. Ni kweli, wanatetea SARE nzuri zao!

    ReplyDelete
  6. Anony wa tatu umesema kweli. serekali ya kikwete inaendekeza ushikaji....jambo lililolalamikiwa mara tu alipoingia madarakani...it is as if sasa wakati wetu wa kula umewadia na tule sasa... it is so sad ukiangalia appointment anaozitoa sasa hivi nyingi zinakwenda kwa vigezo vya uswahiba...bora sasa watu wamejionea athari zake! serekali ya kikwete haikuingia madarakani kwa lengo la kufanya kazi bali kula nchi...ni serekali ambayo mpaka macd wa nguvu wanazuru ofisi za wakubwa saa za kazi...ee Mungu linusuru hili taifa

    ReplyDelete
  7. Wacheni ujinga na chuki nyie hao washikaji gani waliochaguliwa kwenye serikali ya Kikwete si muwataje kwa majina? Juzi kateua makatibu wakuu wapya maana hawa ndio watendai haya tuwaambie ni kina nani washikaji zake?

    Nafikiri watz wengi tunapoenda redio mbao rais hupelekewa majina na watendaji wake pamoja na CV zao majina hayo yanapendekezwa na hao watendaji yeye anakwenda kuithinisha basi na kuwaapisha. Katibu Mkuu kiongozi ndio ana kazi ya kuchagua makatibu wakuu, na wakuu wa mikoa na wilaya hupendekezwa kutoka tawala za mikoa na serikali za mitaa. Aah wacha niachie hapa maana ni sawa na kumwambia kipofu unaona leo jua limewaka!

    ReplyDelete
  8. ccm wote wasengeeeeeeeeee

    ReplyDelete