25 March 2011

CUF yavivyooshea kidole vyombo vya habari

Na Benedict Kaguo

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Julius Mtatiro amedai kuwa baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini vimeandaa mkakati wa
kukidhoofisha na badala yake kukijenga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kionekane chenye uwezo wa kuongoza nchini.

Alisema pamoja na kejeli nyingi zinazotolewa na CHADEMA dhidi ya chama chake, CHADEMA kimekuwa kikipata nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari na kuwadanganya Watanzania kwamba ndicho kinachoweza kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini.

Akihutubia mkutano wa operesheni zinduka katika Uwanja wa Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam juzi, Bw. Mtatiro alisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa ya kupotosha umma kwa kutumia propaganda zinazotolewa na chama hicho dhidi ya CUF.

Alisema ni jambo la kusikitikisha kuona CHADEMA kinaendelea kuishambulia CUF kwa kuiita 'CCM B' badala ya kuikabili CCM lakini baadhi ya vyombo vya habari, bila kuvitaja, vinashindwa kuwaeleza ukweli wananchi juu ya siasa za nchi zinavyokwenda badala yake vimejikita kwenye ushabiki.

Bw. Mtatizo pia aliishambulia CHADEMA kuwa ndiyo yenye uhusiano na CCM kwa kuwa imekuwa ikipokea misaada kutoka kwa wana-CCM, kama Mfanyabiashara Bw. Mustapha Sabodo, na kimekuwa kikiwapokea vigogo wanaokihama chama hicho tawala.

"CHADEMA wamekuwa wakipokea misaada mingi kutoka kwa vigogo wa CCM, mnakumbuka ni juzi tu hapa kada wa CCM Sabodo alitoa milioni 100/- kwa CHADEMA na misaada mingine mingi ambayo haitangazwi, lakini sisi CUF hatujawahi kuwaita CCM B hata siku moja, vigogo wa CCM wanakimbilia CHADEMA na kugombea, hatujasema ni CCM B, lakini leo CUF kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ndio tumekuwa CCM B, na vyombo vya habari vipo haviwaelezi ukweli Watanzania," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kutumika vizuri ili kuwawezesha Watanzania kutambua mustakabali wa taifa lao hasa katika ukuaji wa demokrasia ya kweli.

Awali, Mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohamed alisema wakati akiwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alikubali kushirikiana na CHADEMA kwa kumpa nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Dkt. Willibrod Slaa lakini leo CHADEMA wameunda kambi ya upinzani wanakataa kushirikiana na CUF kwa madai kuwa kwa upande wa Zanzibar wanashirikiana na chama tawala.

"Ndugu zangu chama kilichoshindwa kuwaunganisha watu, kikipewa madaraka kitaongoza kidikteta kwa hiyo nawaomba Watanzania muiogope CHADEMA kama ukoma kwani hakina lengo la kuwasaidia zaidi ya kuchochea ubaguzi," alisema Bw. Rashid

Huku akinukuu gazeti moja la kila siku(sio Majira) Bw. Hamad alisema wakiwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, viongozi wa CHADEMA walitamka hadharani kumpa siku 9 Rais Jakaya Kikwete kuwajibika na kueleza kuwa yaliyotokea Misri yanaweza kutokea nchini.

Alisema kauli hizo hazina nia njema kwa Watanzania kwani amani iliyopo ikitoweka viongozi wa CHADEMA watapanda helkopta na kukimbia na kuwaacha wananchi masikini wakipoteza maisha.

"Sisi CUF tunaamini kuwa tutaindoa CCM madarakani sio kwa mawe, bali kwa hoja nzito za kuwaunganisha wananchi kuwashawishi wakiamini chama chao na hatimaye waweze kukipigia kura kwenye uchaguzi," alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema CCM imegawanyika mapande wawili na pande moja likiona mambo ni magumu linakimbilia CHADEMA na kuwaeleza Watanzania waungane kukiunga mkono CUF ili kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi.

"Ndugu zangu CCM imegawanyika mapande mapande, pande moja linataka kukimbilia CHADEMA na ndio maana vigogo wa CCM wanaisadia mamilioni na wengine kwenda kugombea huko. Kama kuna Watanzania wanaoamini chama cha manyangumi wa ufisadi kinaweza kuleta mabadiliko, ni bora waende Loliondo wakanywe kikombe cha babu maana watakuwa wagonjwa wa akili," alisisitiza Prof. Lipumba.

12 comments:

  1. CUF mlishaisha zamani sana... Toka mmelambishwa uongozi Zanzibar mmekuwa watu wa hovyo sana.
    hatuhitaji CHADEMA kutuambia kuwa nyie ni CCM B. Tunaona matendo yenu, tunasikia matamshi yenu.
    Watanzania sio wapuuzi kiasi hicho mnachofikiri.
    CUF na CCM kuwa na Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar sio tatizo...Tunajua hali ya kisiasa ya Zanzibar ililazimisha hali hiyo. Tatizo ni kuhamishia ndoa hiyo huku bara.
    Badala ya kupigana vijembe na CHADEMA, hata wao hawapaswi kuwatukana majukwaani, tafutaneni mkae chini muondoe tofauti zenu.
    Bila hivyo wote hatuwapi kura 2015... si nyie wala CHADEMA

    ReplyDelete
  2. Tatizo la siasa za TZ lipo katika Udini,ukabila na umangimeza.baadhi ya waandishi wameegemea sana katika ukiritimba huu na mifano ya waziwazi ilionekana wakati wa uchaguzi ulopita.amkeni nanyi sio kulalama katika vyombo vya habari,ukitaka stori yako itoke kwa uzito nyie wenyewe mnajua nini mfanye.tena mna kigezo kimoja kizuri tu hebu onyesheni mfano ZNZ kwa kuibadilisha kimaendeleo ili iwe rahisi na huko BARA kuzidi kuimarika.siasa za huko inaonyesha nyie mpo upande wa kusini na wenzenu wapo nyanda za juu,hivyo basi kuleni nao sahani moja.

    ReplyDelete
  3. Kweli nimebaini kuwa CHADEMA ni CCM B. Maana wanapewa sapoti na CCM. CUF, NGUVU MOJA

    ReplyDelete
  4. Waende kwa babu hao mashabiki wa Chadema wakanywe kikombe cha dawa maana wana kansa ya akili,Chadema imesaidiwa na vyombo vyote vya habari isipokuwa vya serikali bado Watanzania hawakuikubali. CHADEMA NA CCM NI YA WAFANYABIASHARA WATANZANIA TUEPUKANE NAO HASA CHADEMA INA WATU WENYE ASILI YA WIZI TOKA ENZI NA ENZI

    ReplyDelete
  5. Ngugu Mwandishi wa Habari hii,

    We still have long way to go if these are the kinds of comments we hear from Professors of doom and politically handicapped leaders!

    ReplyDelete
  6. Ndugu Mwandishi wa Habari hii,

    We still have a long way to go if these are the kinds of comments we hear from Professors of doom and politically handicapped leaders

    ReplyDelete
  7. Cuf mmenena kweli CHADEMA ndio CCM B wanawazushia tu,hoja yenu nimeilewa vizuri hongereni kwa ufafanuzi huo na kutuweka sawa watanzania

    ReplyDelete
  8. hivi maana yake nini wapinzani kulumbana?
    baada ya kukaa pamoja na kujadili jinsi ya kukiondoa chama tawala (ccm) madarakani mnapigana vijembe wenyewe hebu fanyenyi kitu cha kueleweka na wala sioni tatizo kwa cuf kuwa na serikali ya pamoja na ccm huu ni mwanzo tu,kwani kama hali ya zanzibar itabadirika kiuchumi hapo ndipo wananchi watakapoona kuwa cuf ndio chama kinachostahili kuongoza nchi na wala si ccm kwani ccm imeongoza zaidi ya miaka 40 hakuna kinachoendelea hospitali madawa hakuna umeme wa mgao na mwisho wa siku wanasema kila mwananchi atakula kwa jasho lake.

    ReplyDelete
  9. Kwa nini wasilumbane kama sababu nzuri zipo? Cuf walikuwa viongozi wa upinzani bungeni na walishirikiana na Chadema kwa lengo zuri la kuupa nguvu upinzani kupitia umoja na mshikamano. Sasa hivi Chadema wanaongoza upinzani hawaamini kama kuna chama kingine pinzani, wote ni pandikizi wa Ccm sababu wanazotumia ni dhaifu sana na za kibaguzi. Eti ni sawa kuwahukumu Wazanzibari kwa serikali ya umoja wa kitaifa? Maana maamuzi hayo yalikuwa ni ya wazanzibari kwa mustakabali wao na kila mtu anajua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili. Ni kama Chadema wangependa wazanzibari waendelee kuishi kwa chuki na uhasama, na kama hivyo ndivyo basi wanabakia na sifa gani ya kuongoza nchi kama mbadala wa Ccm? Pengine kuwapa uongozi hawa watu itakuwa ni kama kutoa afadhali na kuweka potelea mbali. Nasisitiza inafaa walumbane, tena wamechelewa sababu nzuri zipo kitambo tu, Chadema ni wabinafsi sana na hilo ni ushahidi kuwa ni waroho wa madaraka tu, hawana nia njema na Tanzania si kwa maneno, nia wala matendo...

    ReplyDelete
  10. mwazo yenu finyu nyie na profeesor wenu uchwara

    ReplyDelete
  11. NGUVU YA UMMA HAIZIMWI KWA MIKUTANO YA USWAHILINI MBAGALA, WAJITOKEZE JANGWANI, KAWE, FURAHISHA MWANZA, NMC ARUSHA, SOKOINE MBEYA UONE KM WATAPATA WATU WA KUWASIKILIZA.

    CCM, CUF, TLP, NCCR, UDP VYOTE VYAIPINGA CHADEMA .

    HII INAMAANISHA CHADEMA NDO CHAMA TAWALA KILICHOCHAKACHULIWA LAKINI KINAONGOZA MIOYO YA WATANZANIA.

    ReplyDelete
  12. RAFIKI WA ADUI YAKO (CUF+CCM=ZNZ) HAWEZI KUWA MWEMA/KUKUTAKIA MEMA HASA HASA UTAKUWA UNAFIKI (CUF+CHADEMA=TANGANYIKA). PROFESA WA WA UCHUMI HAWEZI KUWA AMEBOBEA KWENYE SIASA NDIO MAANA ANAPOTEZA STEP. TUTAFAKARI

    ReplyDelete