02 March 2011

CCM yamtimua mwenyekiti Wazazi Hai

Na Heckton Chuwa, Moshi

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, imemfukuza uanachama wa CCM, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya
chama hicho Wilayani Hai, Bw. James Mushi.

Akielezea sababu ya uamuzi huo jana mjini Moshi, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Stephen Kazidi, alisema uamuzi huo umetokana na Bw. Mushi kutokuwa muadilifu ndani ya chama na kupungukiwa sifa za kimaadili.

"Uamuzi huu umechukuliwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2010, kwenye kifungu cha 93, kifungu kidogo cha 14," alisema.

Akinukuu kifungu hicho cha 14, Bw. Kazidi alisema Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ina wajibu wa kumwachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote endapo itaridhika kwamba tabia yake na mwenendo wake vinamuondolea sifa za uanachama.

"Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa imeridhika kuwa Ndugu James Mushi, tabia yake na mwenendo wake vimemuondolea sifa ya kuwa mwanachama wa CCM," alisema.

Alisema kutokana na uwezo wake wa kikatiba, halmashauri hiyo imemfukuza uanachama Bw. Mushi kuanzia Februari 28, mwaka huu.

Uamuzi huo umekuja miezi kadhaa baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 kumalizika ambapo CCM ilipoteza majimbo kadhaa mkoani humo likiwemo jimbo la Hai ambapo kumekuwa na madai kuwa baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa mamluki jambo lililopelekea kushindwa kwa chama hicho tawala.

Akizungumza na Majira mjini hapa jana, Bw. Mushi alisema hakuwa amepata barua yoyote kutoka ya CCM ikimtaarifu maamuzi hayo, hivyo asingeweza kusema chochote kuhusiana na uamuzi huo.

1 comment:

  1. CCM ACHENI KUSINGIZIA WENGINE KUSHINDWA KWENU NI MAKAMBA NA KIKWETE AKIWEMO GWIJI LA UFISADI ROSTAM...MIKOANI MNAONEANA WENYEWE KWANI JUMUIA ZA WAZAZI NDIO ZINAITA WATU KWENDA MAANDAMANO YA CHADEMA?? FIKIRIA UPYA CHAMA CHOTE KIMEPOTEZA DIRA!!!!!!

    ReplyDelete