Na Amina Athumani
MABINGWA watetezi wa michuano ya Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Business Times 'The Bizze' itafungua pazia la mashindano hayo na
wenyeji NSSF itakayoanza kutimua vumbi Machi 19 mwaka huu.
The Bize katika michuano hiyo imepangwa kundi A na timu za NSSF, Mlimani na Changamoto, wakati kundi B lina timu za Heri Radio, Habari Zanzibar, Global na New Habari.
Kundi C lina timu za Mwananchi, Uhuru, Mwanahalisi, Tumaini na Sahara na kundi D linaundwa na Jambo Leo, TBC, Free Media na IPP.
Katika michuano hiyo ya netiboli, ufunguzi itakuwa kati ya Global na Tumaini ambazo zipo kundi A ambalo lina timu nyingine za Tumaini na NSSF.
Kundi B linaundwa na New Habari, Mwananchi, Free Media na Uhuru wakati kundi C kuna timu za Business Times 'BTL Queens' TBC, IPP na Habari Zanzibar.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kutangaza zawadi za washindi na kukabidhi vifaa kwa timu shiriki, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema mashindano hayo kwa mwaka huu yafanyika kwa mtindo wa ligi kwa mara ya kwanza tofauti na misimu mingingine ambayo ilikuwa mtoano.
Alisema mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka na kushirikisha vyombo vya habari, yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya TCC Chang'ombe na Uwanja wa Chuo cha Uwalimu Dar es Salaam (DUCE).
Alisema kwa mwaka huu mshindi wa kwanza kwa upande wa soka atapata kombe na sh. milioni 3.5, wa pili kombe na sh. milioni 2.5 na wa tatu atapata kombe na sh. milioni 1.5, kwa upande wa netiboli wa kwanza atapata kombe na sh. milioni tatu, wa pili kombe na sh. milioni mbili na wa tatu kombe na sh. milioni moja na mfungaji bora kwa upande wa wanawake na wanaume atapata sh. 200,000 kila mmoja.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Masoud Sanani aliwataka wanahabari kutumia michuano hiyo, ili kujenga kile ambacho wadhamini wa michuano hiyo wamekusudia kwa kuonesha nidhamu pamoja na kuepuka migogoro kwa ajili ya kuziwishi kampuni nyingine kujitokeza.
No comments:
Post a Comment