28 February 2011

Watatu wafa kwa kugongwa na magari

Na Benjamin Masese

WATU watatu wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na magari katika maeneo tofauti huku wengine 43 wakikamatwa na polisi kwa
kosa la kukutwa wakijihusisha na biashara ya bangi na pombe haramu ya gongo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bw. Faustine Shilogile alisema  tukio la kwanza lilitokea juzi saa moja asubuhi babarara ya Ocean eneo la Agha Khan ambapo gari T 126 ATM likiendeshwa na Bw. Athanas John (31) alimgonga mwendesha pikipiki Jongo Sulwa (30) na kumuua, mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na dereva amekamatwa.

Bw. Shilogile alisema kuwa tukio jingine lilitokea juzi saa saba mchana barabara ya Tabata Dampo ambapo gari T669 AAN likiendeshwa na Bw. Hussein Hamis (31) lilishindwa kupanda kilima na kurudi nyuma na kugonga gari lingine lenye namba T 889 AZC aina ya Fuso ambalo liliserereka na kumgonga utingo wake, Ladslaus Njau (32) na kufariki wakati akipelekwa Hospitali ya Amana.

Tukio la tatu lilitokea Barabara ya Mandela ambapo gari lisilofahamika likitoka Buguruni kwenda Feri lilimgonga mtembea kwa miguu mwanamume asiyefahamika mwenye umri kati ya miaka 25 na 30 na kufariki hapo. Mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Amana.

Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Bw. Suleiman Kova alisema watuhumiwa 43 walikamatwa katika msako uliofanywa siku wikendi katika maeneo yanayoaminika kufanyika biashara haramu.

Bw. Kova alisema watuhumiwa hao walikutwa na bangi kilo tatu, kete 38 za dawa za kulevya, misokoto 96 ya bangi pamoja na lita 20 za pombe haramu katika maeneo ya Gymkhanaa-Feri, Mburahati, Kigogo, Manzese, Kibamba, Mbezi Mwisho, Yombo Kisiwani na Dovya .

No comments:

Post a Comment