28 February 2011

Mulugo atoa siku 7 shule ifunguliwe

Na Charles Mwakipesile, Chunya

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo ametoa siku saba kwa uongozi wa idara ya elimu wilaya kuhakikisha  Shule ya
Msingi Itiziro iliyokuwa imefungwa kufunguliwa mara moja ili kuokoa maisha ya wanafunzi ambayo yako hatarini kutokana na kutembelea mwendo mrefu.
 
Bw. Mulugo alitoa agizo hilo akiwa katika ziara yake ya siku 10 kutembelea Wilaya ya Chunya na jimbo lake la Sogwe kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kutimiza baadhi ya ahadi alizoahidi wakati wa kampeni.

Alisema kuwa uongozi wa wilaya hauna budi kutekeleza mapungufu yaliyokuwa yameonekana katika shule hiyo ili kuwafanya wanafunzi ambao sasa wanafuata huduma umbali mrefu kuanza masomo katika shule hiyo kwani makosa yaliyosababisha kufungwa kwa shule hiyo si yao.

Shule hiyo ilifungwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bw. Maurice Sapanjo kutokana na kukosa choo pamoja na nyumba ya mwalimu, na hivyo kuonekana haina sifa ya  kuendelea kutoa huduma hadi wananchi watakapojenga choo na nyumba  ya mwalimu.

Katika kusaidia kukamilisha masharti yaliyokuwa yameifanya shule hiyo kufungwa, Naibu Bw. Mulugo alichangia mabati 70 na mifuko 20 ya saruji ili isaidie kukamilisha ujenzi wa choo na nyumba ya mwalimu. Pia alitoa baiskeli moja kwa ajili ya mwalimu atakayekubali kwenda kufundisha katika shule hiyo.

Kutokana na changamoto hiyo aliutaka uongozi wa Wilaya ya Chunya kuhakikisha unaungana naye kuhakikisha unakamilisha ujenzi huo na ndani ya siku saba shule ifunguliwe.

No comments:

Post a Comment