09 February 2011

Wanafunzi 505 wasimamishwa Tumaini

Na Rehema Maigala

JUMLA ya wanafunzi 505 wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma masomo ya sheria wamesimamishwa masomo katika Chuo Kikuu cha
Tumaini Kampasi ya Kurasini jijini Dar es Salaam kwa kuendesha mgomo kwa wiki moja na nusu na kuandamana kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa chuo, Askofu Alex Malasusa.

Katika taarifa yake kwa vyombo ya habari jana Makamu Mkuu wa Chuo, Bw. Godfrey Mmari, alisema baada ya Kamati ya Uongozi kukaa jana kujadili suala hilo iliamua wanafunzi hao kuondoka chuoni hapo mara moja.

Ilisema kuwa kila mwanafunzi anatakiwa aandike barua kwa Mkuu wa chuo ieleze, kama yupo tayari kuendelea na masomo, mazingira yaliyomfanya ashiriki kwenye mgomo, kumtaja alimshawishi kugoma na kuharibu mali ya chuo na kumpiga mshauri wa wanafunzi kama sio yeye.

Aliongeza kuwa barua hizo zitumwe kwa rejesta (kupitia posta)na zifike kwa Mkuu wa Chuo ifikapo Ijumaa saa 10:30 jioni.

Pia barua hizo zitachambuliwa na wale ambao wataonekana kutokuwa na hatia wataruhusiwa kuendelea na masomo ilimradi watie saini tamko kuwa wanaomba msamaha na hawatarudia tena kugoma.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao walisema kuwa wamekataa kusaini majibu hayo kwa sababu uongozi wa chuo umekataa kutekeleza yale waliyoyataka.

Mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema waliandamana Februari 3, mwaka huu kwa madai ya kutaka kupunguziwa ada, kuboreshewa madarasa, vifaa vya chuo, na kuongezewa walimu lakini hakuna hata jambo moja uongozi huo waliotekeleza.

"Tuliomba kupunguziwa ada kutoka sh. milioni 2.5 na kuwa sh. milioni 1.5 na kuboreshewa huduma zote zikiwa na masomo na za mazingira yanayotuzunguka.

"Lakini uongozi wa chuo hawajafanya hivyo na sisi tukaamua tusisaini hiyo karatasi (isiyokuwa na maboresho) kwa sababu hatujakubaliana nao," alisema.

Alisema kuwa uongozi wa chuo haujawaridhisha kwa kuwa umekataa kushusha ada ya chuo.

Kuhusu suala la mazingira ya chuo ambapo wanafunzi hao walidai kuwa chuo hicho hakina mazingira ya kujisomea.

Alisema uongozi wa chuo uliwajibu kuwa kuhusu hilo wavumiliane kwani wanaandaa mazingira mazuri na kuwaweka walimu sehemu ambayo wakiwahitaji wanawapata kwa haraka.

Baada ya kuwasomea majibu hayo, mkuu wa kitengo cha mafunzo aliwataka mwanafunzi kusaini ili kujua kuwa wamekubaliana nayo au la.

Alisisitiza kuwa mwanafunzi asiyesaini karatasi hiyo atakuwa amejifukuza chuo mwenyewe chuo.

Hata hivyo wanafunzi hao baada ya kupata majibu hayo waliamua kwenda kwa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Kampasi ya Kinondoni na kukuta mlango mkubwa wa kuingilia umefungwa huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia wakiwa pembeni mwa chuo hicho.

1 comment:

  1. jamani tunathamini mchango wa kanisa katika elimu ila ninacchowaomba kanisa muwasikilize hao wanafunzi kwani na wao na wateja na wadau kwakuu wenu,vilevile wanafunzi mjue hicho ni chuo cha private kinajiendesha chenyewe wala serikali yetu haikisadii,tupiganie uhuru wa nchi tupate rais atakaejali elimu ili vyuo binafsi vipewe ruzuku ya kutosha ili kupunguza gharama za masoma/ada

    ReplyDelete