Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA watetezi Simba, jana walitoka kifua mbele katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya kuifunga
African Lyon mabao 3-0.
Katika mchezo huo Simba ilionekana kuwa na uchu tangu mwamuzi alipopuliza kipyenga cha kuanza mechi hiyo, ambapo ilipa bao la kwanza dakika ya tano kupitia kwa Amri Kiemba.
Kiemba alifunga bao hilo baada ya kukutana na mpira uliotemwa na kipa wa African Lyon, Noel Lucas ambaye alikuwa katika juhudi za kuokoa shuti lililopigwa na Jerry Santo ambaye aliunganisha kona iliyopigwa na Rashid Gumbo.
Baada ya kufungwa bao hilo, African mpira ulisimama kwa dakika kumi baada ya kipa Lucas kuumia katika harakati za kuokoa bao hilo.
Mpira ulipoanza baada ya kusimama African Lyon, ilizinduka na kuliandama lango la Simba lakini hata hivyo washambuliaji wake hawakuwa makini katika kuipenya ngome ya Simba iliyokuwa chini ya Meshack Abel.
Hata hivyo Simba nayo katika kipindi hicho cha kwanza ilikosa mabao mengi ya wazi baada ya washambuliaji wake kushindwa kupenyeza mpira wavuni baada ya mara kadhaa kupiga mpira nje.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuingia kwa uchu wa kutaka kufunga na kufanikiwa kupata bao dakika ya 46 kupitia kwa Mbwana Samatta ambaye alikimbia na mpira kuanzia katikati ya uwanja na kuachia shuti lililokwenda nyavuni.
Simba iliendelea kulisakama lango la Lyon kwa kupeleka mashambulizi ya nguvu kutaka kuongeza mabao lakini kama kawaida umakini ulikuwa mdogo.
Mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo waliandika bao la tatu dakika ya 82 kupitia kwa Samatta, ambaye aliunganisha krosi iliyochongwa na Haruna Shamte aliyepanda mbele kusukuma mashambulizi.
Dakika ya 85, Mohamed Banka aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Kiemba alikosa bao la wazi akiwa karibu na lango la Lyon.
Kwa matokeo hayo Simba, sasa imefikisha pointi 30 na kuzidi kuikaribia Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 31.
Waandishi wetu wa habari muwe na uandishi wenye analysis kidogo. Kweli Yanga wanaongoza ligi kwa pointi moja, lakini wapo mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya simba. Vitu vidogo kama hivi kutoviweka kwenye taarifa hupoteza utaalamu wa uchambauzi katika uandishi na taarifa haifurahishi
ReplyDelete