Na Waandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetimiza ahadi yake ya kutoa misaada ya dawa na mashuka kwa waathirika wa milipuko ya
makombora iliyotokea hivi karibuni, katika Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), 511 KJ, Gongolamboto, Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa msaada huo umetokana na ahadi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa na viongozi wengine wa chama hicho, walipowatembelea na kuwapatia pole waathirika hao.
Akikabidhi vifaa hivyo jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Victor Kimesera alisema kuwa chama hicho kinawatakia kila la keri watu wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na milipuko hiyo iliyotokea Februari 16, mwaka huu.
"Ahadi ya vifaa hivi ambavyo ni mashuka 166 na masanduku matano ya dawa vilitolewa na katibu mkuu, Dkt. Slaa, ambaye yuko safarini, hivyo nimekuja hapa kuwakilisha chama kwa niaba yake...tunawatakia kila la heri wagonjwa wote katika hatua mbalimbali za tiba," alisema Bw. Kimesera.
Kwa upande wake Katibu Tarafa wa Ukonga, kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alikishukuru chama hicho kwa kuwajali waathirika wa milipuko hiyo na kuchukulia janga hilo kuwa ni msiba wa taifa, unaopaswa kuwaunganisha Watanzania wote katika majonzi.
Ilielezwa kuwa maboksi hayo matano yamejumuisha dawa zote muhimu na maalumu kwa ajili ya waathirika wa ajali kama hiyo ya milipuko, ambazo zitatumika kwa ajili ya kutibu majeraha.
Hamsini wajitolea damu
zaidi ya wanachama 50 wa chama hicho kutoka Wilaya ya Kinondoni wamechangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa milipuko iliyotokea Gongolamboto ambao wamelazwa katika Hospitali ya Muhimbili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Kinondoni, Bw. Henry Kilewo alisema wameguswa sana na tukio hilo ambalo ni la kitaifa, ndiyo maana wameamua kuchangia damu ili kuwasaidia wagonjwa ambao walipoteza damu nyingi katika milipuko ya mabomu iliyotokea Februari 16, mwaka huu.
"Hili ni janga linalomgusa kila mtu na la kitaifa, naomba watu kuwa roho ya kibinadamu kuwasaidia wahanga hawa.
"Tumeongozana na madiwani na viongozi wengine wa juu wa chama hiki na tunategemea wenzetu kutoka Temeke na Ilala watafika hapa leo (jana) ili kuungana nasi," alisema.
Alitoa mwito kwa vyama vyote vya siasa na taasisi zote nchini kujitokeza kuwasaidia waathirika hao.
Mjumbe wa Baraza la Wanafunzi wa Vyuo vikuu ambao ni wanachama wa CHADEMA (CHASO), Bw. Mugeta Faustine alisema baraza hilo limetoa msaada wa nguo, sabuni, viatu, kilo 50 za unga, mchele na sukari kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha aliwashukuru wote waliojitokeza kuchangia damu ili kunusuru maisha ya waathirika hao.
"Tunatoa shukrani za dhati kwa mwitikio wa Watanzania wote ambao siku tulipotangaza kuhitaji damu walijitokeza kwa wingi kutusaidia. "Siku ya kwanza walijiotokeza watu 107, siku ya pili 100 na bado wanaendelea kujitokeza kutusaidia," alisema.
Imeandikwa Agnes Mwaijega na Tumaini Makene
No comments:
Post a Comment