10 January 2011

Tukivunja amani tukemeeni-Waziri

Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

SERIKALI imeomba madhehebu ya dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuasa viongozi na taifa kwa ujumla pale dalili za uvunjifu wa amani zinapoonekana ili utulivu na amani uendelee kuwepo nchini.Hayo yalisemwa
jana na Bw. Stephen Wassira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu na Uhusiano, wakati wa ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa'ichi.

Bw. Wasira ambaye alitoa salamu binafsi kwa kuongea kwenye ibada, alihudhuria misa hiyo kuwasilisha salamu za pongezi kwa askofu huyo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ujumbe ambao ulikuwa ndani ya bahasha.

"Naliomba Kanisa, mtusaidie kutwambia kuacha pale tunapotaka kuvunja amani pamoja na umoja wetu ambao umedumu kwa muda mrefu. ili nchi iendelee kuwa na amani," alisema Bw. Wassira

Kauli hiyo ya Bw. Wassira imekuja siku moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Arusha kuwakemea viongozi wa dini waliolaani uvunjifu wa amani mkoani humo kwa sababu ya ukiukaji wa taratibu za uchaguzi wa meya, huku wakiweka msimamo wa kutomtambua meya aliyechaguliwa na CCM, Bw. Gaudence Lyimo.

Kutokana na hatua huyo, Katibu wa CCM, mkoani humo, Bi. Mary Chatanda alikaririwa jana akisema maaskofu waliotoa tamko hilo wavue majoho na kujiunga rasmi na siasa.

Lakini jana, Bw. Wasira alionekana kuwa tofauti na msimamo huo, na kuwakaribisha viongozi wa dini kutumia nyadhifa zao kuwakemea viongozi wa siasa wanapopotoka.

Bw. Wassira alipongeza Kanisa hilo kwa mchango wake wa maendeleo kwa nchi, huku akionya kuwa wakati taifa likielekea kutimiza miaka 50 ya Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ya amani iko hatarini kutoweka endapo hatutailinda kwa nguvu zote.

Alisema kuwa watanzania hatuko tofauti na waafrika wengine hivyo tukipenda kuwa na amani tunaweza kwa kuwa jamii ya Watanzania ina waumini wa madhehebu mbalimbali hivyo tukichezea umoja na mshikamano basi amani yetu itatoweka.

Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, alilishukuru kanisa kwa kuanzisha Jimbo jipya la Bunda ambalo alisema litaharakisha maendeleo ya kijamii na kiroho kwa wananchi wa jimbo hilo.Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro akimkaribisha Waziri Wasira, alisema kwamba serikali inahitaji viongozi wa kushirikiana nayo kuongoza watu zaidi ya milioni 3 ili wawaletee maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Awali, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki nchini (TEC), Askofu Mkuu wa jimbo la Songea, Norbert Mtega, alisema waumini wa dhehebu hilo na wananchi kwa ujumla, walinde na kutunza amani, uhuru, usawa na demokrasia ili kuepusha machafuko yanayoweza kutokea nchini.

Askofu Mkuu Mtega alitoa wito huo wakati akitoa salamu za TEC na kuwataka waumini wa madhehebu hayo waufanye mwaka huu wa 2011 uwe wa tafakari ya kina kwa kila mmoja jinsi ya kudumisha uhuru, amani, demokrasia na maendeleo ya nchi.

Akofu Mkuu Ruwa'ichi, akifunga ibada ya misa hiyo alisema kwamba atakuwa tayari kushirikiana na viongozi wa serikali na vyama vya siasa watakaokuwa tayari kutenda haki, usawa na uwazi katika kuwahudumia wanchi.

Wakati huo huo: Papa Mtakatifu Benedict wa XVI amemteua Padre Gervas Naisonga wa Jimbo la Mbeya kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma kushika nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Mkuu Ruwa'ichi.

Naye Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Joseph Chennoth, alisema kwamba hivi sasa kabla ya kusimikwa kwa Padre Naisonga, Askofu Mkuu Ruwa'ichi atakuwa Msimamizi wa Kitume wa jimbo hilo la Dodoma.

1 comment:

  1. Mtoto wako anapokunya kiganjani natumai hutakikata,bali utakiosha kwa maji na kukifanya kiwe safi.Lakini utakapo sikia kuwa mtoto wako mtaani amekuwa mdokozi,Utapiga mbiu ya dhati kwa yeyote ataye muona mtoto huyu anadokoa basi aniarifu ili nimtandike.Je? Ikiwa bwana wassira ulipokuwa kule kilimo kwanza na mkoa wa rukwa kulitokea upotevu wa sh bil 6.0 na mpaka sasa hatujui zilipoishia,????

    Leo hii uwaambie wakuu wa dini wazuie ikiwa kuna fununu za vurugu au fujo,jamani tuangalie ukweli wa nchi yetu hii,si dhani kama kuna mtanzania ambaye anayafurahia maisha haya ya sasa na ndiyo maana wengine wameshayatoa maisha yao kwa wale wote wanaonyonya wenzao.
    Kila bin adam atakufa lakini si kwa style hii ya uhai wako unanyanyasika hivi na rasilimali yako.

    Watanzania pia wamechoka na kauli tamu tata,na utashi wa mali ya asili ya kila anaezaliwa kama mtanzania.

    Inauma wajameni,waziri wetu wa siri kali ya watawala wa tanzanaia.

    ReplyDelete