28 January 2011

Real Madrid, Barcelona zashinda

MADRID, Hispania 

MAHASIMU wakuu nchini Hispania, timu za Real Madrid na Barcelona zinaelekea kukutana kwenye michuano ya Kombe la Mfalme, baada ya wapinzani hao
wakuu kushinda mechi zao za nusu za kwanza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Katika michezo hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia jana, Real Madrid iliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi, Sevilla ikishukuru bao lililofungwa na Karim Benzema

Naye Lionel Messi aliifungia mabao mawili Barcelona ambao ni mabingwa wa mwaka 2009 katika mchezo ambao timu hiyo iliiadhibu Almeria kwa mabao 5-0 katika mchezo huo, uliofanyika kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Vigogo hao wanaofukuzana kwenye michuano ya La Liga na katika michuano ya Kombe hilo la Mfalme, endapo watashinda mechi za pili zitakazofanyika Jumatano wiki ijayo, zitakutana fainali iliyopangwa kufanyika April 20 mwaka huu.

Katika mchezo huo, Sevilla ilikosa magoli mengi huku ikiathirika kwa kupewa kadi nyingi za njano kwenye mechi hiyo ambayo ilifanyika kwenye Uwanja wa Sanchez Pizjuan.

Mbali na hali hiyo, mlinda mlango wa Real Madrid, Iker Casillas naye pia alijikuta akipigwa na kitu kisogoni kilichorushwa kutoka kwa mashabiki wakati akichelewesha dakika lakini hakuumia sana.

Benzema ambaye Jumapili alifunga bao lake la pili msimu huu, aliifanya  Real Madrid iongoze dakika ya 17 mchezo.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa alipachika bao hilo, baada ya kugongeana vizuri na mchezaji Mesut Ozil na kuingia na mpira ndani ya eneo la penalti na kisha kuwalamba chenga mabeki wawili, kabla ya kuachia shuti lililomshinda mlinda mlango, Andres Palop.

Hata hivyo Sevilla, walikaribia kusawazisha bao hilo kabla ya timu hizo kwenda mapumziko wakati mchezaji Luis Fabiano alipomzunguka, Casillas lakini akapiga mpira uliotoka nje ya goli wakati lango likiwa tupu.

Katika mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nou Camp, mchezaji Pedro aliipatia bao Barcelona dakika ya 30  likiwa ni bao lake la nne msimu huu.

Hata hivyo mchezaji bora wa Dunia, Messi ndiye aliyeipatia bao la kuongoza timu yake dakika ya tisa na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Hispania, David Villa akaongeza la pili dakika mbili baadaye na Messi akapiga la tatu dakika 16 ya mchezo.

Kipigo hicho ni cha pili kwa Barcelona kuichapa Almeria, baada ya mapema msimu huu timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 8-0.

No comments:

Post a Comment