20 January 2011

Polisi adaiwa kupora gari, fedha

Na Glory Muhiliwa, Arusha

MTU anayesadikiwa ni askari polisi mwenye sare za jeshi hilo, huku akiwa na silaha aina ya SMG, amempiga risasi ya shingo dereva taksi mmoja na kumjeruhi vibaya na kusababisha alazwe katika chumba cha
wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Selian mjini hapa.

Taarifa za tukio hilo zimeeleza kuwa, askari huyo,  alifika katika eneo la Shivaz, Kaloleni mjini hapa, Januari 17, mwaka huu, majira ya saa 10 usiku, na kumtaka dereva huyo ampeleke katika Kituo cha Polisi cha Ngarenaro baada ya makubaliano ya kulipwa sh. 3,000.

Imeelezwa kuwa mara baada ya kufika karibu na kituo hicho, askari huyo alimwamuru dareva huyo kusimamisha gari lake lenye namba T.976 AGZ aina ya Toyota Mark 11, na kumtaka ampatie chenji sh. 7,000 ili yeye (askari) ampe noti ya sh. 10,000.

Wakiwa na askari huyo wakielekea Ngarenaro, inadaiwa kuwa kila muda askari huyo alikuwa akiwasiliana kwa simu muda wote na wenzake.

Wakati dereva huyo aliyetambulika kwa jina la Jamal Abdul(32) akijaribu kutoa fedha hizo, askari huyo aliyekuwa ametoka nje ya gari, alikoki silaha yake na kumfyatulia risasi moja iliyompata sehemu ya shingo na kutokeza upande wa pili, pia ilimjeruhi katika bega la kushoto.

Dereva huyo aliyekuwa akizungumza kwa taabu hospitalini hapo, alisema anamtambua mtu huyo kuwa ni askari polisi na kwamba mara baada ya kukumbwa na masahibu hayo, aliamua kufika katika kituo hicho cha polisi Ngarenero, kuomba msaada.

"Cha kushangaza mara baada ya kufika kituoni hapo, askari waliokuwa zamu siku hiyo waligoma kunifungulia mlango na kunitaka niende Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa kwa ajili ya kupata msaada zaidi," alisema Jamal.

Habari zaidi zinasema kuwa baada ya kumjeruhi dereva huyo, askari huyo alipora gari hilo na kuelekea eneo la Mbauda, ambapo alifanya tukio la uporaji wa fedha katika kituo kimoja cha mafuta, akiwa na wenzake.

Inadaiwa pia baada ya tukio la uporaji, askari huyo na wenzake, waliondoka kwa kasi na gari hilo, hata hivyo aligonga gari aina ya Toyota Hiace eneo la Mbauda, ambapo alilitelekeza gari na kutokomea kusikojulikana.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio walidai kuwa mfuko huo wa fedha ulikuwa ukidondosha sarafu barabarani, huku askari huyo na wenzake wakiendelea kukimbia wakiwa na sare za polisi.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Bw. Thobias Andengenye alikiri kupata taarifa hizo na kwamba wanafanya uchunguzi."Tutatoa taarifa juu ya tukio hilo, bado tunafanya uchunguzi kubaini ni askari gani alihusika na tukio hilo, maana inawezekana pia siyo askari, bali majambazi waliamua kuvaa sare ili kujifanya polisi," alisema Bw. Andengenye.

Hata hivyo familia ya majeruhi, waliokutwa wodini hapo, ambao hawakutaka kutajwa majina, walililalamikia Jeshi la Polisi kwa kushindwa kutoa ushirikiano juu ya tukio hilo, japo wanakiri kuwa baadhi ya viongozi wa jeshi hilo, wamefika hospitalini hapo kumjulia hali majeruhi huyo.

No comments:

Post a Comment