28 January 2011

Mshtakiwa augua, aanguka kizimbani

Na Rabia Bakari

MSHTAKIWA katika kesi ya kutapeli fedha kwa njia ya udanganyifu, Bi. Mwadawa Abdallah ameanguka na kuzimia kizimbani baada ya presha
kupanda na sukari kushuka ghafla wakati akisomewa mashtaka yake.

Tukio hilo lilitokea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi ya Bi. Abdallah ilipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Agustina Mbando.
 
Awali baada ya kuitwa mahakamani, mshtakiwa aliingia na kuelekezwa sehemu ya kusimama, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama, Bw. Zuberi Mukakatu, alianza kumsomea mashtaka mawili yanayomkabili, ambayo ni kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Alikana mashtaka yote, na wakati taratibu za kimahakama zikiendelea, ghafla alisikika akiomba msaada wa kushikwa mkono na askari aliyekuwa karibu, akidai kuwa anasikia kizunguzungu na ataanguka wakati wowote.

Hakuna aliyemshika mkono mwanamke huyo, na badala yake walimwelekeza kwenye benchi lililokuwa mahakamani hapo na kumtaka akae, alipolifikia alilala na ghafla alidondoka kutoka katika benchi hilo hadi chini, huku akiwa hajitambui na kurusha mikono.

Hata hivyo, Hakimu Mbando aliendelea na taratibu za kimahakama kwa kupanga tarehe ya kutajwa kesi baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi haujakamilika, ambapo pia mahakama ilisema dhamana ipo wazi.

Mshtakiwa huyo huku akiwa chini, Hakimu alisema anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, watakaosaini hati ya sh. milioni tano, sambamba na kuwa na hati ya mali isiyohamishika, ambapo aliwataka wadhamini wajitokeze kama wapo.

Wakati zoezi la kusubiri wadhamini likiendelea, walijitokeza askari wa kike waliombeba mama huyo na kumtoa nje, ambapo mahakama iliahirishwa na watu wote kutoka nje.

Hadi gazeti hili linaondoka mahakamani hapo, hali ya mama huyo bado ilikuwa mbaya, ambapo ndugu zake walionekana wakilia huku wakitafuta msaada wa huduma ya kwanza.

Katika mashtaka ya msingi, alidaiwa kuwa mnamo Januari 21 mwaka huu, katika maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo akiwa na wenzake ambao bado hawajakamatwa walijipatia zaidi ya milioni 10.5, mali ya Nuru Bakari kwa madai ya kumpatia pampu za maji kitu ambacho walijua si kweli. Kesi hiyo itatajwa tena Februari 10 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment