21 January 2011

Milioni 500/- zatengwa kuboresha dampo Pugu

Na Heri Shaaban

SERIKALI imetenga sh. milioni 500 kwa ajili ya kuboresha dampo la Pugu Kinyamwezi ili kunusuru  afya ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwaepusha na magonjwa ya
milipuko.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Bakari Kingobi, wakati wa mahojiano katika kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1).

Bw. Kingobi alisema kuwa dampo la Pugu lina zaidi ya miaka mitano, lakini afya za wakazi wa eneo hilo zipo hatarini  kutokana na mrundikano wa taka zinazopelekwa hapo na  uduni wa vitendea kazi.

"Bajeti ya mwaka 2011/2012 tumeandaa fedha hizo kwa ajili ya kununua kijiko ili  kupunguza mrundikano wa taka ambazo zinaingia kila siku, " alisema Bw. Kingobi.

Kwa mujibu wa Kingobi, wanatarajia kukopa fedha kutoka Benki ya NMB ili waweze kununua mitambo ya kisasa itakayotumika katika dampo hilo na fedha hizo zinatarajiwa kupatikana miezi sita ijayo.

Awali takataka zilikuwa zikitupwa dampo la Tabata lakini baada ya kuongezeka kwa taka,  Serikali ilisitisha utupaji wa taka na kuhamishia Mtoni ambapo pia halikuchukua muda na kuhamishiwa Pugu Nyamwezi.

No comments:

Post a Comment