Na Elizabeth Mayemba
WAANDAAJI wa mechi za kirafiki za kimataifa kati ya timu ya Atletico Paranaence ya Brazil na Yanga, wametangaza viingilio kwamba vitakuwa sh. 200,000 kwa VIP A na cha chini sh. 5,000.Viingilio hivyo ambavyo viliwahi
kutumika katika mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na timu ya taifa ya Brazil, pia vitatumika keshokutwa kati ya Simba na Wabrazil hao.
Akitangaza viingilio hivyo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya African Lyon ambayo ndiyo waliyoileta timu hiyo, Nabil Alkharous alisema viingilio vingine kwa jukwaa la VIP B ni sh. 100,000, VIP C sh. 50,000, orange sh. 20,000, nyuma ya magoli sh. 10,000 na viti vya bluu sh.5,000.
"Tunaimani viingilio hivyo vimeendana na mechi yenyewe na pia kila shabiki atapata nafasi ya kufika uwanjani kwa kuwa kiingilio cha chini kabisa tumeweka sh. 5,000 ambacho mashabiki wengi watamudu," alisema Alkharous.
Akizungumzia mchezo wa leo Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic alisema wamejiandaa vizuri japo kuwa timu yake inakabiliwa na majeruhi wengi.
"Pamoja na kwamba kikosi changu kinamajeruhi wengi, nitaingiza timu yangu uwanjani kwa kuwa mchezo huu ni muhimu kwa sisi tunaojiandaa na michuano ya kimataifa," alisema Papic.
Alisema endapo wachezaji wake waliopo kwenye timu ya taifa 'Taifa Stars' waliopo Misri kwenye michuano ya Bonde la Mto Nile watawahi kurudi nchini wataungana na wenzao.
Naye kocha wa Simba, Patrick Phiri aliwapongeza waliodhamini ziara ya timu hiyo na kwamba wachezaji wake watatumia mchezo huo kupata uzoefu katika michuano inayowakabili."Ni kipimo kizuri kwetu na tunawapongeza sana wenzetu wa African Lyon, kutuletea timu hii ambayo itatusaidia katika maandalizi ya michuano inayotukabili," alisema Phiri.
Timu hiyo iliwasili nchini mwishoni mwa wiki kwa ziara ya michezo miwili ya kirafiki.
No comments:
Post a Comment