Na John Daniel
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), wamegoma kuingia darasani kuendelea na masomo kushinikiza serikali kulazimisha uongozi wa chuo hicho kuwarudishia fedha zao vinginevyo wataandamana hadi
ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete kudai haki zao.
Wamesema serikali inawajibika kuhahakisha wanarudishiwa fedha zao kwa kuwa watendaji wake walishiriki kutoa taarifa za uwongo juu ya uhalali wa chuo hicho, hivyo kuwafanya walipe mamilioni ya fedha kinyume na hali halisi.
Wakizungumza na Majira chuoni hapo jana, wanafunzi hao walisema serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ndiyo iliyowaingiza katika matatizo ya kulipa fedha zao kinyume cha utaratibu, hivyo ni lazima iwajibike kuhakikisha wanalipwa.
"Tunachotaka ni serikali kulazimisha uongozi wa chuo kuturudishia fedha zetu zote tulizolipa, tulidahiliwa kupitia mfumo wa TCU na wao walisema wanatambua, hiki ni chuo Kikuu, kama hawataki tutaandamana hadi kwa rais ikulu," alisema Bw. Aman Manengelo.
Wanafunzi hao walisema baada ya kubaini chuo hicho kutokuwa na hadhi ya kuwa chuo kikuu kama walivyotaarifiwa awali, wamechukua hatua kadhaa kuiomba serikali kuwasaidia lakini watendaji wake wanawazungusha bila kuwapa jibu sahihi.
"Baada ya matatizo kuanza, TCU wameiondoa hata kwenye mtandao wao lakini zamani ilikuwepo, hivi kweli nchi hii imefikia ufisadi mpaka kwenye elimu jamani, au hii ni DECI nyingine," alihoji Bw. Kusanja Emmanuel.
Akielezea jinsi walivyoshughulikia suala hilo kabla ya kufikia hatua ya sasa, mwakilishi wa wanafunzi hao, Bw. Byson Charles alisema walibaini uwongo wa KIU walipofika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
"Tupo kama wanafunzi 400 tulioingia hapa kupitia mfumo rasmi wa TCU, tulipofuatilia mikopo, Bodi ya Mikopo walitujibu kuwa chuo chetu hakitambuliki, hivyo hawawezi kutukopesha kama vyuo vikuu vingine.
"Baada ya hapo tulienda TCU wakashindwa kutupatia jibu la uhakika, tulipoenda Wizara ya Elimu na Ufundi ndio wakakiri kuna makosa walifanya, lakini waziri w akashindwa kutoa jawabu ya nini kifanyike, ndio maana sasa tumefikia hapa," alisema Bw. Charles.
Bw. Charles alikiri Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia suala hilo na kwamba alipewa taarifa kutoka vyombo vya usalama kuwa watapatiwa majibu ya mwisho Jumatatu wiki ijayo, japo hawana uhakika.
Wanafunzi hao waliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza usajili wa KIU kuanzia ilipoingia nchini na kuweka wazi kuwa wanawasiwasi kuwa wahusika walikula rushwa kuweka taarifa za uongo kinyume na vigezo vya TCU.
Majira ilishuhudia gari la Polisi namba PT 2094 ikiwa imewasili chuoni hapo na askari zaidi ya sita waliokuwa tayari kukabiliana na tisho lolote la amani huku Mkuu wao akiwa kwenye kikao ndani ya Ofisi za Utawala wa KIU.
Msimamizi wa wanafunzi wa Chuo hicho, Bw. Marco Allute alithibitisha kujua madai hayo ya wanafunzi na kueleza kuwa yanashughulikiwa.
"Hivi sasa niko kwenye kikao kama ulivyona na tunajadili suala hilo hilo, naomba muda nipigie simu baadaye tunaweza kuongea zaidi," alisema Bw. Allute.
No comments:
Post a Comment