17 December 2010

Waliotajwa kuhusika na ghasia Kenya wadai hawana hatia

NAIROBI,Kenya

MUDA mfupi  baada ya Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC)Bw. Luis Moreno Ocampo kuwataja watu sita wanaoshukiwa kuwa wahusika wakuu katika ghasia zilizozuka baada ya  baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007 nchini Kenya, viongozi wametoa hisia zao.

Miongoni mwa viongozi waliotoa maoni yao ni pamoja na Rais Mwai Kibaki ambaye alisema kuwa  watu hao sita waliotajwa, wakiwemo mawaziri wawili na Mkuu wa Utumishi wa Umma, bado hawajafanyiwa uchunguzi wa kutosha kwa sababu shughuli hiyo ya kuwashtaki haijaanza rasmi huko The Hague.


Rais Kibaki aliongeza kuwa wito uliotolewa na Bw. Ocampo kutaka washukiwa hao sita kuchukuliwa hatua una madhara na unakwenda kinyume na haki zao za kimsingi. Naye Meja Jenerali Hussein Ali, ambaye alikuwa Mkuu wa Polisi alisema alifanya majukumu yake ipasavyo na kwamba mashtaka dhidi yake hayana msingi.

Wengine pia waliotupilia mbali tuhuma dhidi yao ni Bw.Uhuru Kenyatta ambaye ni Waziri wa Fedha, Bw.William Ruto ambaye ni  Waziri wa zamani wa Elimu ya Juu na Bw. Francis Muthaura Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini humo ambao walisema kuwa madai hayo hayana msingi wowote na wakasema kwamba wapo tayari kwenda kusimama mbele ya mahakama hiyo.Hatua hiyo imekuja baada ya juzi Bw. Ocampo kuwataja watuhumiwa hao kuhusika katika ghasia hizo zilizozuka  mara baada ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Waliotajwa jana na Ocampo ni  Naibu Waziri wa Fedha,Bw. Uhuru Kenyatta,Waziri wa Viwanda,Bw. Henry Kosgey,Waziri aliyesimamishwa kazi,Bw.William Ruto,Mkurugenzi wa redio,Bw. Joshua Arap Sang,Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri,Bw. Francis Kirimi Muthaura  na Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi,Bw. Mohammed Hussein Ali.

Watu takribani 1,200 walipoteza maisha na wengine zaidi ya  500,000 walizikimbia nyumba zao ili kukimbia mapigano hayo.Katika harakati za kutafuta amani zilizofuatia,ilikubaliwa kwamba wahusika wakuu wa kuchochea ghasia hizo wangekumbana na sheria nchini Kenya ama katika Mahakama hiyo ya ICC mjini The Hague.

Hata hivyo wabunge wa Kenya walizuia kuanzishwa mahakama maalumu nchini humo na mapema Jumatatu wiki hii Rais  Mwai Kibaki akatangaza kuwa Serikali itafanya uchunguzi wake tangazo ambalo linadaiwa kuonekana kama ni kutaka kuzuia watuhumiwa wasifikishwe mjini  The Hague.

Tayari Jeshi la Polisi nchini humo limeshajiweka katika hali ya tahadhari endapo inaweza kutangazwa kutokea tena hali ya machafuko.Inaelezwa kuwa  watuhumiwa wote sita watakabidhiwa barua za kuitwa mahakamani wenyewe na endapo watashindwa kufanya hivyo ama kuficha ushahidi mfano kwa kuingilia mashuhuda Bw. Ocampo  atalazimika kuomba waraka ili wakamatwe.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza,BBC anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki,Bw. Will Ross anasema kuwa katika siku za hivi karibuni kulikuwepo na kiwewe miongoni mwa wanasiasa ambao huwa hawaguswi.(BBC).

   

No comments:

Post a Comment