02 December 2010

Waliokosa viti maalumu waangua kilio

Na Patrick Mabula, Kahama

BAADHI ya Madiwani wa Viti Maalumu katika Wilaya ya Kahama wiki hii walijikuta wakiangua kilio baada ya  kukosa uteuzi kutokana na asilimia waliyopata katika uchaguzi uliomalizika Oktoba 31, mwaka huu.Madiwani hao ambao huingia kwenye
Baraza la Madiwani kutokana na asilimia ya wingi wa madiwani wanaogombea kwenye kata walijikuta wakiangua kilio majina yao hayamo
katika orodha ya asilimia ya wateuliwa.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kahama Bw. Sospeter Nyigoti alisema chama kilikuwa na madiwani wa viti maalumu 19 waliokuwa wamepita katika mchakato wao.

Bw. Nyigoti alisema kama CCM ingekuwa imeshinda katika kata zote za Wilaya ya Kahama kwa asilimia mia madiwani hao wa viti maalumu wageingia wote, lakini ilipoteza baadhi ya kata hali iliyofanya asilimia kupungua na kufanya waliopata nafasi kuwa 14.

Kutokana na hali hiyo madiwani watano walikosa nafasi ndipo waliokuta majina yao hayamo kwenye orodha uvumilivu uliwashinda na kuangua kilio mbele ya wanzao.

Wilaya ya Kahama ina majimbo mawili ya uchaguzi la Msalala na Kahama na ina jumla ya kata 55 ambapo katika uchaguzi mkuu uliomalizika wapinzani walipata kata 13 na CCM ilishinda kata 42 na kufanya wapinzani kupata viti maakumu vitano.

No comments:

Post a Comment