10 December 2010

EPZA yang'ara uwekezaji Afrika

Na Mwandishi Wetu 
    
MAMLAKA ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Tanzania (EPZA) imepewa dhamana ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kanda Huru za Uwekezaji Afrika (AFZA)

utakaofanyika Machi mwakani jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa sekta hiyo kutoka nchi tofauti duniani.

Tanzania imependekezwa na Benki ya Dunia (WB) kwa kushirikiana na AFZA baada ya kuridhishwa na hatua za kiutendaji za EPZA nchini zilizoifanya nchi husika kuwa na mafanikio makubwa kiuwekezaji katika kipindi kifupi cha utendaji wake tangu kuanzishwa.

EPZA Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya utendaji wake imetengeneza ajira zaidi ya 10,000, pato la kigeni la zaidi ya sh. bil 300 na kutenga maeneo ya uwekezaji kwa zaidi ya mikoa 14 nchini.

Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Katibu Mkuu wa AFZA, Bw. Chris Ndibe aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kusaidia utekelezaji wa shughuli za EPZA na kufikia mafanikio waliyonayo, hadi Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika shughuli za uwekezaji Afrika.

Alisema kuwa nchi wanachama wa AFZA wamefurahishwa na juhudi zinazofanywa na EPZA Tanzania na kuipendekeza kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaojumuisha zaidi ya wajumbe 250 kutoka nchi wanachama wa AFZA na WFZC.

Ripoti ya kiutendaji ya EPZA Tanzania iliyotolewa na Benki ya Dunia katika mkutano wa kwanza wa AFZA uliofanyika Nigeria mwaka huu, ndio iliotoa ushawishi kwa mamlaka hizo kuipendekeza Tanzania kuandaa mkutano huo.

"Ufanisi wa kiutendaji wa EPZA Tanzania ndio kigezo cha sisi kuipa nafasi hiyo nyeti ambayo kwa namna moja itaendelea kuchagiza maendeleo ya Sekta ya Uwekezaji
kwa nchi husika," alisema Bw. Ndibe.

Aliongeza kuwa pamoja na kupewa uenyeji wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru alichaguliwa kuwa Balozi wa WFZC kwa nchi za Afrika Mashariki katika mkutano wao uliofanyika Falme za Kiarabu mwezi uliopita.

Akizungumzia mafanikio hayo, Dkt. Meru alisema kuwa yamechangiwa na mambo mengi ambapo mchango wa serikali umekuwa chachu kubwa ya ufanisi wao.

Alisema serikali katika kipindi cha miaka minne ya utendaji wa EPZA ilitenga zaidi ya sh. bil 20 ambazo zimesaidia kulipa fidia na hatimaye kupatikana kwa
maeneo ya uwekezaji katika maeneo tofauti nchini.

"Tunaishukuru serikali kwa mchango wanaotupatia kwa kipindi cha miaka minne ambapo tumeweza kuendesha shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa eneo maalumu la
uwekezaji la Benjamin William Mkapa Special Economic Zones (BMW-SEZ)," alisema Dkt. Meru.

Akizungumzia mkutano utakaofanyika nchini mwakani alisema wanatarajia kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiufundi na nchi wanachama utakaosaidia kuleta tija na ufanisi wa kazi ndani ya sekta ya uwekezaji nchini.

No comments:

Post a Comment