10 December 2010

Taifa Queens yazidi kung'ara Singapore

Na Amina Athumani

TIMU ya taifa ya Tanzania ya netiboli ´Taifa Queens´ imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya Kimataifa yanayofanyika nchini Singapore, baada ya kuifunga India kwa
magoli 60-27.

kwa mujibu wa taarifa zilizoletwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Simone Macknis kwa njia ya simu jana alisema timu yake ilionesha umahiri mkubwa katika mchezo huo, ambapo hadi mapunziko ilikuwa mbele kwa mabao 38-12.

Taifa Queens iliwatumia wafungaji wake warefu vizuri kupachika mabao hayo, ambapo Mwanaidi Hassan alifanikiwa kupachika mabao mengi zaidi na kuifanya Tanzania kuongoza katika vipindi vyote viwili vya mchezo huo.

Kocha huyo alikisifu kikosi chake kwa kiwango kikubwa ilichokionesha  katika mchezo huo na kumpongeza nahodha wake, Jacline Skozi kwa kuzuia mashambulizi ya nguvu ya wapinzani wao yaliyokuwa yakielekezwa langoni mwao.

Timu hiyo ya Tanzania ilitarajiwa kushuka tena uwanjani jana jioni kucheza na Namibia, kabla ya kumenyana na Wales kutafuta nafasi ya kuingia robo fainali, ambayo itachezwa Jumapili.

Hadi sasa timu inayoongoya katika michuano hiyo kwa kushinda michezo yote mitatu iliyocheza ni timu ya Scotland ikifuatiowa na Tanzania pamoja na wenyeji wa michuano hiyo Singapore, ya tatu Wales ya nne Namibia na ya mwisho India.

No comments:

Post a Comment