10 December 2010

Kili Stars leteni raha leo

Na Zahoro Mlanzi

MACHO na masikio ya wadau wengi wa soka, leo yataelekezwa katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano ya Kombe la Chalenji, kati ya wenyeji Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' itakayooneshana
kazi na mabingwa watetezi Uganda 'The cranes'.

Mbali na mchezo huo, nusu fainali nyingine itaanza kupigwa saa tisa alasiri itakayozikutanisha Ivory Coast itakayoumana na Ethiopia, michezo yote hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kili Stars iliingia hatua hiyo baada ya kuichapa Rwanda, bao 1-0 na Uganda iliing'oa Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-3.

Kocha Mkuu wa Kili Stars, Jan Poulsen akizungumzia mchezo huo mara baada ya kumalizika dhidi ya Rwanda juzi, alisema haiwazii sana Uganda ila atakachofanya ni kuendelea na mazoezi.

"Ukiwa kocha hutakiwi kuzungumza kila kitu, ninachowaomba Watanzania wawe na moyo wa subira na wajitokeze siku hiyo (leo), kuja kuona timu yao, kwani kuwepo kwao uwanjani kutawapa hamasa kubwa," alisema Poulsen.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Uganda, Bobby Williamson alisema atahakikisha wanatetea ubingwa wao kwa kutinga fainali, kwani anakiamini kikosi chake kutokana na jinsi wanavyocheza.

"Katika mashindano haya, naheshimu timu zote zilizoshiriki hivyo hakuna tutakayoidharau, tutakakichofanya ni kuhakikisha tunashinda mchezo huo," alisema Williamson.

Kwa upande wake Ivory Coast, yenyewe ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Malawi bao 1-0 na Ethiopia, ambao ni mabingwa mara nne wa michuano hiyo iliichapa Zambia mabao 2-1.

Mchezo huo nao unatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake, hasa ikizingatiwa kwamba Ivory Coast ni timu iliyoonesha kandanda safi kwa kucheza mpira wa chini huku, Ethiopia wao wakionekana ni timu dhaifu hasa ilipoingia robo fainali, baada ya kuwa na matokeo mazuri (best looser), hivyo itataka kudhihirisha uwezo wao kwamba hawajabahatisha.

No comments:

Post a Comment