24 December 2010

Real Madrid yaiadhibu Levante 8-0

BARCELONA, Hispania

WACHEZAJI Cristiano Ronaldo na Karim Benzema, usiku wa kuamkia jana waliibuka mashujaa baada ya kuifungia Real Madrid mabao matatu kila mmoja yaliyoifanya timu hiyo, kuibuka na ushindi mnono wa mabao 8-0 dhidi ya
Levante katika raundi ya 16 ya michuano ya Kombe la Copa del Rey, 'Kombe la Mfalme'.

Kwa mabao hayo kwa sasa Ronaldo, amefikisha mabao 25 katika mechi  24 alizoichezea Real Madrid katika michuano yote ya msimu huu.

Mbali na wachezaji hao, wachezaji Mesut Oezil na Pedro Leon waliifungia mabao moja moja.

kikosi hicho kinachonolewa na kocha Jose Mourinho, katika mchezo huo wa kwanza kuucheza kwenye Uwanja wa Santiago Bernebeu, tangu kilipoonesha kiwango cha chini na kufanikiwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya ligi dhidi ya Sevilla, iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Matokeo ni mazuri kwa upande wetu na mashabiki wetu, kwa sababu wanapenda kuona soka na ninaamni tumelionesha," alisema  Benzema, ambaye katika kampeni zake amefikisha mabao tisa.

Katika mtanange huo, Benzema alipachika bao la kwanza dakika ya sita baada ya kuipenya ngome na kisha kumchambua mlinda mlango, Gustavo Munua kwa shuti hafifu na Oezil akaipatia Real Madrid bao la pili, baada ya  Ronaldo kunasa mpira karibu na mstari wa katikati ya uwanja na kisha kukimbia nao kabla ya kumpasia Mjerumani huyo, ambaye alikuwa karibu na eneo la penalti.

Benzema aliipatia bao la tatu Real Madrid, dakika ya 32 baada ya kuingia eneo la hatari na kumalizia pasi aliyomegewa na mchezaji Angel Di Maria, kabla ya Mfaransa huyo kumtengea pasi  Ronaldo, akiwa ndani ya yadi sita kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.

Alikuwa tena Benzema aliyemtungua Munua dakika ya 70, baada ya kupokea pande safi kutoka kwa Di Maria kabla ya Ronaldo, kupachika mabao mengine dakika ya 72 na 74 huku, Leonel Messi akishindilia msumari wa mwisho dakika ya 90.

Baada ya mchezo huo, Mourinho alisema ameridhika na jinsi Benzema alivyocheza kuliko alivyofunga mabao.

“Alikuwa akifanya jitihada za kuwasaidia wenzake na kuhakikisha anautafuta mpira, pindi alipokuwa akiupoteza,” alisema kocha huyo Mreno.

No comments:

Post a Comment