16 December 2010

Papic: Mwape, Kijiko mtawaona Jumamosi

Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Mserbia Kostadin Papic,  amesema kwamba, uwezo wa wachezaji wake wapya Mzambia Davies Mwape na Juma Seif 'Kijiko', utaonekana Jumamosi wakati timu hiyo itakapojipima na Azam FC.Timu hizo mbili zinakutana
katika mchezo wa kirafiki, kwa ajili ya kutambulisha vifaa vyao, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mwape na Kijiko, walisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili kwa ajili ya kuongeza nguvu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania na michuano ya kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Papic alisema uwezo wa wachezaji wake hao utaonekana katika mechi hiyo ya kirafiki, kwani lazima awapange ili awaone.

"Najua hata mashabiki wa timu yetu watakuwa na shauku kubwa ya kuwaona wachezaji hawa kama wataisaidia timu yetu au la, lakini ni matumaini yangu kuwa, watafanya vizuri," alisema Papic.

Timu hiyo, jana jioni ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru, baada ya kumaliza mazoezi ya viungo 'gym'.Awali, Yanga walikuwa waanze mazoezi jana asubuhi, lakini timu ya Azam FC ikawa tayari uwanjani, hivyo wakapanga kufanya jioni.Wakati Yanga ikianza mazoezi ya uwanjani, mahasimu wao Simba, bado wanaendelea na mazoezi ya ufukweni kwa ajili ya kutafuta stamina.

Wiki mbili zilizopita, Simba walikuwa wakifanya mazoezi ya viungo 'gym' na sasa wamehamia ufukweni chini ya kocha wao Mkuu Patrick Phiri.

No comments:

Post a Comment