22 December 2010

Nyota ya Liyumba yafifia

Na Grace Michael

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania jana ilitupilia mbali rufani ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Bw. Amatus Liyumba na kuamuru kubaki uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.Hukumu hiyo ilitolewa mahakamani hapo na Jaji Emiliana Mushi ambapo alisema kuwa haoni sababu ya kubadili uamuzi huo kwa kuwa ulifikiwa baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha makosa ya mshitakiwa huyo bila shaka yoyote na adhabu iliyotolewa ilikuwa  sahihi.

"Mahakama haikukosea kutoa uamuzi ambao iliufikia na mimi sioni sababu ya kuingilia kilichoamuliwa ambacho kilizingatia ushahidi wa pande zote mbili," alisema.

Bw. Liyumba kupitia wakili wake Bw. Majura Magafu alipinga uamuzi uliokuwa umefikiwa na Jopo la Mahakimu watatu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo Mei 24 mwaka huu ambao walimtia hatiani katika makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela.

Katika sababu zake za rufaa, alidai kuwa Mahakama ya Kisutu ilishindwa kuangalia kwa kina ushahidi uliotolewa hatua iliyoifanya ikafikia uamuzi huo na pia ilishindwa kutumia vigezo vilivyopo katika kutoa hukumu ambapo ilitakiwa kutumia kigezo cha faini au kifungo kwa kuwa sheria inaruhusu hivyo.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mushi alisema kuwa hakuna ubishi kuwa Bw. Liyumba na aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu  Daud Balali walihusika katika mradi huo wa majengo pacha na mabadiliko ya mradi huo yalifanywa bila kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi huku wakijua taratibu za Benki hiyo.

"Taratibu za BoT zilikuwa wazi ambapo kabla ya kufanya chochote ni lazima idhini itoke katika Bodi ya Wakurugenzi lakini wao walipuuza na kuendelea kufanya mabadiliko hayo na baadae kuomba idhini hivyo walifanya kinyume na taratibu zilizokuwepo," alisema Jaji Mushi.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha bila kuacha shaka yoyote katika makosa aliyotiwa nayo hatiani hivyo haoni sababu ya kubadili uamuzi huo.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Bw. Magafu anayemwakilisha Bw. Liyumba alisema kuwa anatarajia kukata rufani katika Mahakama ya Rufaa kwa kuwa upande wao hawakuridhishwa na hukumu iliyofikiwa na Mahakama Kuu.

Awali Bw. Liyumba alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya ofisi  ambayo alidaiwa kuwa kati ya mwaka 2001 na 2006 akiwa jijini Dar es  Salaam, alitumia vibaya mamlaka ya ofisi yake kwa kuchukua uamuzi wa mabadiliko ya mradi wa majengo pacha uliokuwa ukijulikana kama 10 Mirambo bila kuwa na idhini ya Bodi ya Wakurugenzi.

Mbali na kosa hilo pia alikabiliwa na kosa la kuisababishia  Serikali hasara ya sh. bilioni 221.1 ambazo zilitokana na mabadiliko aliyoyafanya bila ya kuwa na idhini kama zilivyokuwa taratibu za BoT.

Kutokana na mashitaka hayo, kwa kipindi chote cha kesi, mshitakiwa huyo hakuwahi kupata dhamana kutokana na masharti magumu yaliyokuwa yametolewa ambapo alitakiwa kuweka nusu ya fedha alizodaiwa kuingiza hasara mahakamani.

Hata hivyo, baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka kumaliza kutoa ushahidi wao, Bw. Liyumba hakuwa na kesi ya kujibu katika shitaka la pili hivyo alibaki na kosa la matumizi mabaya ya ofisi ambalo lilimfanya akutwe na hatia Mei 24, mwaka huu na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

1 comment:

  1. Liyumba ndiyo ametolewa kafara ionekane wapo seriouse na kupambana na rushwa! Mwache amalizie tu muda wake Imebaki miezi 12 atoke akendelee na maisha yake!

    Tatizo la huyu bwana ni kubeba wanawake wa wenzake aliingia pabaya kwa wakubwa sasa ndo wamemvika kesi ya rushwa na imemkaa kweli kweli kama suti ya Ulaya! Si anamuona mwenzake Babu Seya?!

    Asingekuwa hivyo pengine leo angekuwa " Mwenzetu" "Ndugu yetu" pale Halmashauri Kuu au CC.

    Nchi hii!!! Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firau!

    Aka mi sipo!!!!

    ReplyDelete