17 December 2010

Majambazi yateka kijiji yaua Mfanyabiashara

Na Faida Muyomba,Chato

WA T U k u m i w a n a o s a d i k i w a kuwa majambazi wamemuua kwa risasi mfanyabiashara mmoja na kujeruhi wengine kadhaa katika kata ya Buselesele wilayani Chato, mkoani Kagera kisha kuwapora zaidi ya sh. milioni 7. Majambazi hayo
yaliendesha operesheni hiyo kwa zaidi ya saa mbili katika vijiji vya Buselesele, Mapinduzi na katika kijiji cha Katoro kilichoko wilayani Geita ambapo kabla ya tukio hilo yalifyatua risasi kadhaa angani na kurusha bomu la moto.
Aliyeuawa katika tukio hilo lililotokea jana saa 8 usiku, ni Bw. Joseph Munis (40) mfanyabiashara wa viatu ambaye alipigwa risasi mgongoni na nyingine kisogoni ambapo licha ya kumuua yalimpora sh. milioni 3.2.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi katika mahojiano kwa njia ya simu na gazeti hili, alithibitisha kuwepo tukio hilo ingawa alisema alikuwa hajapata taarifa kamili.
“Ni kweli tukio hilo lipo hivi sasa nasubiri taarifa kamili kutoka kwa RCO aliyeko kwenye eneo la tukio, hivyo nipigie baadaye, “alisema kamanda huyo lakini hata hivyo Majira lilipomtafuta baadaye, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alieleza kuwa kamanda huyo alikuwa kwenye kikao cha dharura kwa Mkuu wa Mkoa.
Wakizungumza na Majira katika eneo la tukio, baadhi ya wananchi walisema kuwa majambazi hayo kabla ya kupora na kuua, yalifyatua risasi kadhaa angani pamoja na kurusha bomu la moto ambapo watu walijificha majumbani na hakuna aliyethubutu kutoka nje.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la  Bw. Robert Elias (28) ambaye chumba chake kipo jirani na cha marehemu alisema; “Nilisikia risasi nje, nyingine ikasikika jirani kabisa na mlangoni, nikataka nitoke lakini roho ilisita niliingia uvunguni na kumwacha mke wangu peke yake.”
Aliendelea kueleza baada ya muda kidogo, alishtukia watu hao wakiingia chumbani kwake na kumwamuru mkewe awape fedha na kudai hana ndipo wakaanza kupekua chumba kizima na walipokosa wakaondoka ndipo alisikia kelele kwa mpangaji mwenzake.
Naye Bi.Anna Masanyiwa ambaye ni shemeji wa marehemu alisema kuwa watu hao walipofika walivunja mlango wa chumba alimokuwa amelala na kuuliza mahali alipo Bw. Munis ambapo aliwaonesha.
Wakati akiwaonesha kumbe marehemu na mkewe tayari walikuwa wamesikia sauti hizo, yalipofika alijaribu kuzuia mlango ndipo yalimfyatulia risasi na kufa papo hapo kisha kupora kiasi hicho cha fedha. Majambazi hayo yalimjeruhi pia mfanyabiashara mwingine katika nyumba hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Bw. Sadiki na kumpora zaidi ya sh.laki nane na baadaye yalipora tena kwa Bw.Tawaqal Charles.
Mbali na kumpora Bw. Charles ambaye ni mfanyabiashara wa duka la nyama katika kijiji cha Mapinduzi ,yalimjeruhi kichwani na sehemu mbalimbali za mwili huku yakimtishia kumkata kwa shoka ambapo pia yalimjeruhi mkewe Bi. Naomi Emmanuel na mtoto aitwaye Matokeo ambapo yalikuwa yakidai kupewa sh. milioni 10.
Diwani wa Kata ya Buselesele, Bw. Chrispine Kagoma, aliliambia Majira kuwa alijikuta akidondosha simu yake ya mkononi kutokana na mlio wa bomu lililorushwa na kusababisha hofu kwa wananchi. Diwani huyo alisema kuwa ipo haja kwa wananchi kuanza kufanya doria za mara kwa mara kudhibiti uhalifu huo huku akilitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kuwalinda raia wake badala ya kulinda vituo pekee.
Habari zinasema kuwa majambazi hayo yaliendesha uhalifu huo katika kijiji cha Katoro ambacho ni jirani na Buselesele na kupora zaidi ya sh.laki 5 kabla ya kutokomea baada ya polisi kutoka kituo cha Buselesele na Katoro kufika eneo hilo.

3 comments:

  1. Du,hii imekuwa ni war zone.Inabidi pia polisi wapewe moyo,wanapofanaya kazi nzuri wapongezwe na wananchi wajulishwe,juzi juzi askari wa Tabora walijitoa muhanaga na kupambana hadi kuua majambazi 5 hatujasikia jeshi likito pongezi zozote kama ilivyokuwa zamani,pia Geita tulisikia jinsi polisi walivyopambana kishujaa na majambazi watekaji na kuwaua watano,hatujasikia jeshi ilo likitoa pongezi au medali yoyote kwa kitendo hico,nakumpuka wakati wa IGP aliyepita alikuwa akitembelea askari waliofanaya kitendo cha kishujaa na kuwapa zawadi na pongezi kwa huyu anaona ni wajibu wao,nadhani hii inabidi aliangalie ili kuwapa moyo askari shujaa wanao amua kujitoa muhanga kupamabana na majambazi.

    ReplyDelete
  2. Kuna vitu vingine ni aibu kuvisikia kwa nchi ambayo inajiita nchi yenye amani na upendo?Sasa ikiwa kijiji kinatekwa na kijiji hiki kimo ndani ya nchi yenye amani na upendo sidhni kama maana ya haya maneno amani na upendo yamepewa hadhi yake kupewa Tanzania. Wajibu wao ni kuwalinda wananchi na sio kusubiri tukio kisha kupewa zawadi,Hii itawafanya kuwa na katabia kachafu.Kosa lao hawa askari wetu ni kuwa hawalindi wananchi bali vituo vyao na nyumba za waheshimiwa pia mafisadi wa nchi na mali zao.
    Inforcement ya hawa polisi wetu haina mpangilio tuu

    ReplyDelete
  3. Napenda kutoa maoni yangu kuhusu JANGA LA MAJAMBAZI hii ni fedheha kubwa kwa nchi kama TANZANIA yenye amani kwa muda mrefu na kwa kipindi hichi ndiyo mambo yanazidi kuwa mabaya
    Mapenda kutoa shauri langu kwa JESHI LA POLISI na kwa wananchi wote waungane pamoja na kurudishe ushirikiano ule wa zamani la kuunda vikundi vya kulinda amani katika kila mji kwa jina la KIKOSI CHA SUNGUSUNGU ambalo lilikuwa likisaka kila mjeni angiaye katika mji wao bila kujulikana na wenyeji wa mji. Yaani huyu mgeni sio maarufu ni kusudi gani limemleta hapo? Naona jambo hili litaleta amani katika miji mbali mbali kama litatekelezwa. Mimi Hilal Masaud Al Jabri toka Maskati Oman.

    ReplyDelete